Swali: Tunaona kwa kiasi kikubwa kuenea kwa laana kati ya watu wengi kutokana na sababu ndogo. Kama kumlaani mtu kwa dhati yake, kuwalaani wazazi wawili na ndugu. Tunaomba utubainishie ukhatari wa jambo hilo juu ya dini ya muislamu.

Jibu: Kumlaani muislamu pasi na haki ni dhambi kubwa au ni miongoni mwa maasi yaliyodhihiri. Ikiwa kuwalaani ni wazazi wawili basi dhambi inakuwa kubwa na khatari zaidi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Kumlaani muumini ni kama kumuua.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika walaanaji hawatokuwa mashahidi wala waombezi siku ya Qiyaamah.”

Ameipokea Muslim katika ”as-Swahiyh” yake.

Pia amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Kumtusi muislamu ni dhambi nzito na kumuua ni ukafiri.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Alisema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwaambia Maswahabah wake:

“Je, nisikujuzeni juu ya madhambi makubwa zaidi?” Wakasema: “Ndio, ee Mtume wa Allaah.” Akasema: “Kumshirikisha Allaah, kuwaasi wazazi wawili, kusema uongo” au alisema “kushuhudia uongo.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Hapana shaka kwamba kuwalaani wazazi wawili ni utovu mbaya kabisa. Kwa hivyo ni lazima kwa waislamu wote kwa jumla na khaswa kwa watoto juu ya wazazi wao kujichunga kutokana na jarima hili na kutakasa ndimi zao kutokamana na jambo hilo hali ya kuwa ni wenye kutahadhari kutokamana na ghadhabu na adhabu ya Allaah na huku ni wenye kupupia juu ya kubaki kwa mapenzi na udugu kati ya muislamu na ndugu zake na kati ya mtoto na wazazi wake. Namwomba Allaah awawafikishe waislamu juu ya kila kheri.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (07/148)
  • Imechapishwa: 21/03/2021