Wasiwasi katika wudhuu´ na namna ya kujitibu

Swali: Mimi ni mwanamke ambaye ninatilia mashaka sana juu ya usahihi wudhuu´. Utaniona nikirudi kutia wudhuu´ upya mara nyingi mpaka nikapatwa na kukata tamaa juu ya usahihi wa wudhuu´. Dawa ni ipi?

Jibu: Dawa ni kwamba kila mtu anatambua ni mara ngapi anatakiwa kuosha viungo vyake. Akiosha mara moja inatosha. Akiosha mara ya pili ndio kamilifu. Akiosha mara ya tatu ndio kamilifu zaidi. Akiosha kwa mara ya nne, basi itambulike kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayezidisha juu ya hapo… “

Bi maana zaidi ya mara tatu.

“… basi amefanya vibaya, amevuka mipaka na amedhulumu.”

Je, hivi kweli wewe unapenda kusifika kwa sifa hizi; kufanya vibaya, kuvuka mipaka na kudhulumu? Hakuna yeyote anayependa haya. Kwa ajili hiyo unatakiwa kuutegua mtego wa shaytwaan. Utakapoosha mara tatu basi toka hapo unapofanya wudhuu´ na mtake msaada Allaah na uswali. Mimi nakubali kwamba yule ambaye amepewa mtihani wa wasiwasi huu shaytwaan atamwambia kwamba bado hajaswali, hajatekeleza faradhi, hajatekeleza nguo miongoni mwa nguzo za Uislamu na kwamba ukifa juu ya hali hii basi umekufa juu ya yasiyokuwa maumbile. Atamng´oneza ibara kama hizi. Lakini azipuuze. Amtake msaada Allaah kwa kusema:

أعوذ بالله من الشيطان الرجيم

“Najilinda kwa Allaah kutokamana na shaytwaan aliyefukuzwa mbali.”

Atambue kuwa Allaah (Ta´ala) anajua na atamuuliza ni kwa nini alizidisha juu ya yale yaliyothibiti kutoka kwa Mtume wako (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni yepi yaliyothibiti kutoka kwa Mtume; je, ni mara tatu au ni mara ishirini? Ni mara tatu. Ataulizwa siku ya Qiyaamah. Ni kipi kilichokufanya ukazidisha juu ya yale yaliyopokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Wewe ni mbora au yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Je, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifanya upungufu katika kukufikishia? Hapana, hakupunguza. Yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitawadha mara moja-moja, mara mbili-mbili na mara tatu-tatu. Lengo ilikuwa kuwabainishia Ummah wake kwamba yote hayo yanafaa.

Kwa ajili hiyo tunamwambia mwanamke huyu amche Allaah juu ya nafsi yako. Komeka katika mara tatu na zipuuze zile wasiwasi zinazokuja moyoni mwako kwamba wudhuu´ wangu haukutumia na kwamba swalah yangu haikutimia. Puuzilia mbali wasiwasi wa shaytwaan. Hili litakuwa zito kwako kwa muda wa wiki moja, wiki mbili, mwezi mmoja au miezi miwili. Kuyatendea kazi haya itakuwa ni kazi ngumu kidogo, lakini mtake msaada Allaah na simama kidete dhidi ya adui wa Allaah na mtake msaada Allaah kabla ya kila kitu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (51) http://binothaimeen.net/content/1155
  • Imechapishwa: 27/06/2019