Wasemayo hawa kina dada wa Kenya ni sahihi?


Swali: Anasema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Swalini kama mlivyoniona mimi nikiswali”.

Kinachofahamika katika Hadiyth hii ni kuwa, hakuna tofauti kati ya Swalah ya mwanaume na ya mwanamke. Sawa katika kusimama, kuinama, Rukuu´ wala Sujuud. Kwa ajili hii, mimi huwa sitofautishi, lakini huku kwetu baadhi ya wanawake Kenya wananikasirikia na kunambia kuwa Swalah yangu sio sahihi kwa kuwa inafanana na Swalah ya mwanaume. Na wanataja dalili ambazo – kwa mtazama wao – zinatofautisha Swalah ya mwanaume na ya mwanamke; kama kuweka mikono juu ya kifua au kuiacha na namna ya kushutama katika Rukuu´ na yasiyokuwa hayo katika mambo ambayo sikukinaika nayo. Naomba unibainishie; je, Swalah ya mwanaume na ya mwanamke katika utekelezaji kuna tofauti?

Jibu: Uliyosema dada muulijizaji, sahihi ni kuwa hakuna tofauti kati ya Swalah ya mwanamke na Swalah ya mwanaume. Na waliyosema baadhi ya wanach-uoni ya utofautishaji hayana dalili. Na Hadiyth uliyoisema katika swali lako, nayo ni kauli yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Swalini kama mlivyoniona mimi nikiswali”.

Inahusu watu wote. Shari´ah za Kiislamu zinawahusu wanaume na wanawake, isipokuwa yaliyo na dalili ya ukhusishaji. Sunnah ni mwanamke kuswali kama anavyoswali mwanaume; sawa katika Rukuu´, Sujuud, usomaji, uwekaji wa mikono juu ya kifua, hivi ndio bora. Hali kadhalika, jinsi ya kufanya Rukuu´, jinsi ya kufanya Sujuud katika ardhi, yanayosemwa katika Rukuu´ na Sujuud, baada ya kutoka katika Rukuu´ na Sujuud ya kwanza, yote haya (mwanamke) ni sawa kama anavyofanya mwanaume.Kwa kuifanyia kazi dalili ya maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Swalini kama mlivyoniona mimi nikiswali”. (Swahiyh al-Bukhaariy)

Muulizaji: Kuhusiana na kudhihirisha kisomo na kukimu Swalah, je, Swalah ya mwanamke siinatofautiana na ya mwanaume katika hili?

Jibu: Kukimu kunatoka nje ya haya, ´Iqaamah na adhaana ni khususan kwa wanaume tu. Kuna maandiko ya haya. Wanaume wanaadhini na wanakimu, ama wanawake hawana kukimu wala kutoa adhaana. Ama kudhihirisha (yaani kusoma kwa sauti) anaweza kusoma kwa sauti; Fajr, Maghrib na ´Ishaa. Rakaa mbili za asubuhi, na Rakaa mbili za mwanzo za Maghrib na ´Ishaa anaweza kusoma kwa sauti kama wanavyofanya wanaume.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/4025/%D9%84%D9%8A%D8%B3-%D8%A8%D9%8A%D9%86-%D8%B5%D9%84%D8%A7%D8%A9-%D8%A7%D9%84%D8%B1%D8%AC%D9%84-%D9%88%D8%B5%D9%84%D8%A7%D8%A9-%D8%A7%D9%84%D9%85%D8%B1%D8%A7%D8%A9-%D9%81%D8%B1%D9%82
  • Imechapishwa: 12/03/2018