Wanajengea hoja maneno ya Abu Haniyfah juu ya Zakaat-ul-Fitwr


Swali: Wale wanaojuzisha kutoa Zakaat-ul-Fitwr mali wanajengea hoja kwamba Imaam Abu Haniyfah (Rahimahu Allaah) amejuzisha jambo hilo. Kipi kinachosemwa kwao kwa kuzingatia kwamba kitendo hicho kinapingana na Hadiyth Swahiyh za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?

Jibu: Tunawaambia:

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

“Mkizozana juu ya jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamuamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri kabisa.”[1]

Tatizo la watu hawa ni kwamba hawatambui thamani ya Qur-aan na Sunnah. Dogo niwezalo kusema ni kwamba hawatambui thamani ya Qur-aan na Sunnah ukilinganisha na wanavotambua thamani walionayo maimamu. Jengine ni kwamba wanayatazama madhehebu haya manne kana kwamba ni Shari´ah nne zilizowekwa ambapo inafaa kwa muislamu kuchukua chochote katika hayo anachotaka. Watu aina hii wanahitajia mtu awatolee muhadhara awafunze maana ya dini. Je, dini ni maoni ya watu au dini ni kama alivosema Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah):

Dini ni kunukuu aliyosema Allaah, Mtume Wake na Maswahabah

ndio wanazuoni

Elimu sio kujinasibu mwenyewe kipumbavu

kwenye tofauti kati ya Maandiko na maoni ya mtu[2]

Ni wajibu wafahamu kwamba masuala yote ambayo wanachuoni wametofutiana basi yanatakiwa yarudishwe katika Qur-aan na Sunnah. ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alifaradhisha kutoa Swaa’ ya tende au Swaa’ ya ngano kuwa ni Zakaatul-Fitwr iliyowajibika kwa waislamu wote; mtumwa aliye huru, mwanamume, mwanamke, mtoto mdogo na mzee na kwamba itolewe kabla ya watu kwenda kuswali.”[3]

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefaradhisha Zakaat-ul-Fitwr ili mfungaji atwaharishwe na ujinga na magomvi ili kuwalisha masikini. Mwenye kuitoa kabla ya swalah basi ametoa zakaah yenye kukubaliwa na mwenye kuitoa baada ya swalah ametoa swadaqah miongoni mwa swadaqah.”[4]

Makusudio ya swadaqah hii ni kulisha chakula, kwa ushahidi wa Hadiyth hii. Warudi wazitazame Hadiyth hizi; Hadiyth ya kwanza inapambanua ni chakula kipi kinachotakiwa kutolewa na Hadiyth ya pili inabainisha hekima ya kufaradhishwa chakula hicho.

[1] 04:59

[2] Kutoka katika shairi ”an-Nûniyyah” la Imaam Shams-ud-Diyn bin Qayyim-il-Jawziyyah.

[3] al-Bukhaariy (1503) na Muslim (984).

[4] Abu Daawuud (1609), Ibn Maajah (1827), ad-Daaraqutwniy (2/138) na al-Haakim (1/409) ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye. Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Abiy Daawuud” (1420).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naasir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Hudaa wan-Nuur (317)
  • Imechapishwa: 21/05/2020