Wanafunzi wa kiume kusoma kwenye klasi moja na wanafunzi wa kike na kupeana mikono


Swali: Ni ipi hukumu kwa mwanamke kuwasalimia wanafunzi wenzake darasani kwa kupeana mikono? Ni ipi hukumu endapo yeye mwanamke atanyoosha mkono wake kumsalimia?

Jibu: Haijuzu kusoma kwa kuchanganyikana na wasichana sehemu moja au klasi moja. Hii ni katika sababu kubwa za mtihani. Haijuzu kwa wanafunzi wa kiume wala wa kike ushirikiano huu kutokana na ile mtihani inayopatikana ndani yake.

Haifai kwa muislamu kupeana mikono na mwanamke ambaye sio Mahram wake hata kama atamnyooshea mkono. Badala yake anatakiwa kumweleza kuwa kupeana mikono na wanaume ambao sio Mahram zako haifai. Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema katika mnasaba wa kuwapa bay´ah wanawake:

“Hakika mimi sipeani mikono na wanawake.”[1]

Imethibiti vilevile kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ya kwamba amesema:

“Ninaapa kwa Allaah ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwahi hata siku moja kupeana mikono na wanawake. Hakuwa anapa bay´ah isipokuwa kwa maneno tu.”[2]

Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا

“Hakika mna kigezo chema kwa Mtume wa Allaah kwa yule mwenye kumtaraji Allaah na siku ya Mwisho na akamdhukuru Allaah kwa wingi.” (33:21)

Jengine ni kwa sababu mtu kupeana na wanawake ambao sio Mahram zake ni miongoni mwa njia za fitina. Kwa hivyo ni wajibu kuachana na jambo hilo.

Kuhusu kupeana salamu iliyowekwa katika Shari´ah ambayo haina fitina pasi na kupeana mikono, mashaka, kulegeza sauti na wakati huohuo mtu akawa amejisitiri vizuri na isiwe sehemu ya faragha hakuna neno. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

يَا نِسَاءَ النَّبِيِّ لَسْتُنَّ كَأَحَدٍ مِّنَ النِّسَاءِ ۚ إِنِ اتَّقَيْتُنَّ فَلَا تَخْضَعْنَ بِالْقَوْلِ فَيَطْمَعَ الَّذِي فِي قَلْبِهِ مَرَضٌ وَقُلْنَ قَوْلًا مَّعْرُوفًا

“Enyi wake wa Mtume!  Nyinyi si kama yeyote yule katika wanawake. Hivyo basi mkimcha [Allaah], basi msilegeze kauli asije akaingiwa tamaa ambaye moyoni mwake mna maradhi na semeni kauli inayotambulika.” (33:32)

Sababu nyingine ni kwa kuwa wanawake katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa wakimtolea salamu na wakimuuliza maswali katika yale mambo yanayowatatiza. Vivyo hivyo wanawake walikuwa wakiwauliza Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika mambo yanayowatatiza.

Kuhusu mwanamke kupeana mikono na wanawake wenzake na wanaume ambao ni Mahram zake kama vile baba yake, kaka yake, mjomba wake na Mahram wengineo hakuna neno.

[1] an-Nasaa´iy (4181), Ibn Maajah (2874), Ahmad (06/357) na Maalik (1842).

[2] al-Bukhaariy (4891), Muslim (1866), Abu Daawuud (2941) na wengineo.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (04/247)
  • Imechapishwa: 13/08/2017