Wanachuoni wa Ahl-us-Sunnah kuhusu kuswali nyuma ya mtenda dhambi

Ikiwa sio mtawala ndiye mwenye kuongoza Ijumaa na idi, bali ni imamu aliyeteuliwa na nchi au kukawa hakuna imamu mwingine na huyu aliyewekwa ni mtenda dhambi, kunaswaliwa nyuma yake au hakuswaliwi? Jibu ni kwamba kunaswaliwa nyuma ya mtenda dhambi katika hali mbili:

Hali ya kwanza: Ikiwa huyu ndiye mtawala wa waislamu na watu hawana imamu mwingine isipokuwa huyu. Yule anayeswali peke yake na akaacha kuswali nyuma yake, Ahl-us-Sunnah wanaonelea kuwa ni mzushi.

Hali ya pili: Ikiwa tendo hilo halitopelekea katika uharibifu kwa kuacha kuswali nyuma yake. Kwa mfano kukatokea mizozo kati ya waislamu na fitina na chuki.

Ama kukiwa kuna imamu mwingine na hilo halipelekei katika uharibifu ukaswali nyuma yake na ukaacha kuswali nyuma ya imamu ambaye ni mwadilifu, hapa ndipo wanachuoni wametofautiana kama swalah inasihi au haisihi.

Hanaabilah na Maalikiyyah wanaonelea kuwa swalah si sahihi na ni wajibu kurudi kuiswali tena. Shaafi´iyyah na Ahnaaf wanaonelea kuwa swalah ni sahihi pamoja na kwamba imechukizwa. Hii ndio kauli sahihi. Sahihi ni kwamba swalah inasihi pamoja na machukizo. Dalili ya hili ni yale yaliyothibiti katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy kupitia Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wawaswalisheni – yaani maimamu wenu – wakipatia, wana fungu lao na nyinyi mna fungu lenu, na wakikosea, mna fungu lenu na wao hawana kitu.” al-Bukhaariy (694).

Hadiyth hii inaonesha wazi kuwa imamu akikosea kosa linampata yeye mwenyewe. Ama kuhusu maamuma hawapati kitu katika hilo.

Vilevile imethibiti kuwa Maswahabah walikuwa wakiswali nyuma ya al-Hajjaaj bin Yuusuf na alikuwa ni mtenda dhambi na dhalimu. Kadhalika Maswahabah waliswali nyuma ya Waliyd bin ´Uqbah bin Abiy Mu´aytw ambaye alikuwa ni kiongozi wa Kuufah kabla ya ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh). Mtu huyu alikuwa ni mtenda dhambi anakunywa pombe. Mpaka siku moja aliwaswalisha Fajr na alikuwa amelewa ambapo aliwaswalisha Rakaa nne kisha akawageukia na kuwauliza:

“Mnataka niwazidishie?” ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) akamwambia: “Tangu tuko na wewe hujapatapo kuzidisha!”

Halafu akarudi kuswali tena na akaenda kumshtaki kwa kiongozi mkuu akampiga bakora na kumwondosha.

Imethibiti pia katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy kwamba ´Uthmaan bin ´Affaan (Radhiya Allaahu ´anh) watu wa mapinduzi walimtinga nyumbani kwake kutaka kumuua – watu hawa ni mafusaki – ilipofika wakati wa swalah akatangulia mbele mtu mmoja wa mapinduzi na kutaka kuwaongoza watu. Ndipo akaja mtu na kumuuliza kiongozi wa waumini ´Uthmaan kwa kumwambia:

“Ee kiongozi wa Mtume wa Allaah! Muda wa swalah umefika sasa na kuna mtu mmoja katika watu wa mapinduzi anataka kutuongoza katika swalah. Je, tuswali nyuma yake ilihali ni mtenda dhambi?” Akamwambia: “Ee ndugu yangu! Hakika ya swalah ni miongoni mwa vitu bora wanavyofanya watu! Akifanya vizuri nanyi fanyenyi vizuri pamoja naye na endapo ataharibu basi jiepusheni na kuharibu kwake.” al-Bukhaariy (695).

Maandiko haya yanafahamisha kuwa kuswali nyuma ya mtenda dhambi ni sahihi na hairudiliwi. Lakini hata hivyo ni jambo lisilokuwa na shaka kwamba lililo bora ni kuswali nyuma ya mtu ambaye ni mwadilifu.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (01/530-531)
  • Imechapishwa: 19/05/2020