Walinganie manaswara kwa Qur-aan na Sunnah – hapana Biblia

Swali: Kuna bwana mmoja amehifadhi Injiyl. Anawalingania manaswara katika Uislamu bali mpaka kujadiliana nao kupitia vitabu vyao. Je, kitendo hicho kinafaa kwake?

Jibu: al-Bukhaariy amepokea kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Msiwasadikishe Ahl-ul-Kitaab na wala msiwakadhibishe. Ima mkasadikisha kilicho batili au mkakadhibisha kilicho haki.”

Udhahiri  wa nyongeza ”Ima mkasadikisha kilicho batili au mkakadhibisha kilicho haki” haiko katika al-Bukhaariy. Ibn ´Abbaas pia amesema:

”Kitabu chenu ndio kipya zaidi kilichotoka kwa Mola wenu. Je, mmemuona yeyote kutoka katika Ahl-ul-Kitaab akikuulizeni kitu?”

Kwa hivyo sio mfumo wa sawa. Allaah (´Azza wa Jall) amesema katika Kitabu Chake kitukufu:

فَبِأَيِّ حَدِيثٍ بَعْدَ اللَّـهِ وَآيَاتِهِ يُؤْمِنُونَ

“Basi maneno gani baada ya Allaah na Aayah Zake wataamini?”[1]

Pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anapowalingania makafiri wa Quraysh, basi anawasomea Qur-aan. Jubayr bin Mutw´im alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na huku akamkuta anaswali swalah ya Maghrib na anasoma Suurah “at-Twuur” mpaka alipofika katika maneno Yake (Ta´ala):

أَمْ خُلِقُوا مِنْ غَيْرِ شَيْءٍ أَمْ هُمُ الْخَالِقُونَ  أَمْ خَلَقُوا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۚ بَل لَّا يُوقِنُونَ

“Au wameumbwa pasipo na kitu chochote au wao ndio waumbaji au wameumba mbingu na ardhi? Bali hawana yakini.”[2]

Jubayr amesema kuwa alikuwa bado hajakuwa muislamu na ndipo moyo wake ukakurubia kuruka. Katika upokezi mwingine amesema kwamba ndipo imani ilipoingia ndani ya moyo wake.

Nakunasihini muwalinganie watu kwa Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] 45:06

[2] 52:35

  • Mhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://muqbel.net/sounds.php?sound_id=38 Tarehe: 1420-11-17/2000-02-22
  • Imechapishwa: 09/01/2021