Wakeze Mtume wanaingia katika watu wa nyumbani kwake


1761 – Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Enyi watu! Hakika mimi nimekuachieni kitu ambacho endapo mtashikamana nacho basi kamwe hatompotea; Kitabu cha Allaah na jamaa zangu wa karibu wa nyumbani kwangu.”

Ameipokea at-Tirmidhiy na at-Twabaraaniy kupitia kwa Zayd bin al-Hasan al-Anmaatwiy, kutoka kwa Ja´far, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Jaabir bin ´Abdillaah.

Ni jambo linalotambulika kwamba Shiy´ah wanatumia sana hoja kwa Hadiyth kiasi cha kwamba baadhi ya Ahl-us-Sunnah wanafikiria kuwa ni wenye kupatia katika nukta hiyo. Hata hivyo ni wenye kukosea kwa pande mbili:

1- Jamaa wa karibu wa nyumbani ni wengi zaidi kuliko wanavokusudia Shiy´ah. Ahl-us-Sunnah hawalikatai hilo, kinyume chake, ni wenye kushikamana nalo. Jamaa zake wa karibu ni wale  watu wa nyumbani kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama ilivyobainishwa katika Hadiyth. Wanaoshika msitari wa mbele kabisa katika jamaa zake wa karibu ni wake zake, akiwemo yule ambaye ni Mkweli mno ´Aaishah – Allaah awawie radhi wote. Hayo yamesemwa wazi katika maneno Yake (Ta´ala):

يَا نِسَاءَ النَّبِيِّ لَسْتُنَّ كَأَحَدٍ مِّنَ النِّسَاءِ ۚ إِنِ اتَّقَيْتُنَّ فَلَا تَخْضَعْنَ بِالْقَوْلِ فَيَطْمَعَ الَّذِي فِي قَلْبِهِ مَرَضٌ وَقُلْنَ قَوْلًا مَّعْرُوفًا

“Enyi wake wa Nabii!  Nyinyi si kama yeyote yule katika wanawake; mkimcha Allaah, basi msilegeze kauli asije akaingiwa tamaa ambaye moyoni mwake mna maradhi na semeni kauli inayokubalika.”[1]

Kisha Akasema:

وَقَرْنَ فِي بُيُوتِكُنَّ وَلَا تَبَرَّجْنَ تَبَرُّجَ الْجَاهِلِيَّةِ الْأُولَىٰ ۖ وَأَقِمْنَ الصَّلَاةَ وَآتِينَ الزَّكَاةَ وَأَطِعْنَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا

“Tulizaneni majumbani mwenu na wala msijishauwe kwa kuonyesha mapambo kama walivyojishauwa zama za ujahili na simamisheni swalah na toeni zakaah na mtiini Allaah na Mtume Wake. Hakika si venginevyo Allaah anataka akuondosheeni maovu, enyi watu wa nyumbani kwa Mtume, na akutakaseni mtakaso barabara.”[2]

Kule Shiy´ah kukhusisha Aayah hii juu ya ´Aliy, Faatwimah, al-Hasan na al-Husayn (Radhiya Allaahu ´anhum) na kuwaondosha wakeze (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ni aina fulani ya kuipotosha Qur-aan na kwa ajili ya kutaka kuyanusuru matamanio yao.

2- Jamaa wa karibu wanalengwa wale wanachuoni na waja wema ambao wameshikamana na Qur-aan na Sunnah. Imaam Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Jamaa wa karibu ni wale watu wa nyumbani kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao wanafuata dini yake na wameshikamana na maamrisho yake.”

[1] 33:32-33

[2] 33:33

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah (4/654-655)
  • Imechapishwa: 05/08/2021