Wake zangu wote wawili hawaswali, nifanye nini?


Swali: Mimi nimeoa wanawake wawili, lakini wote wawili hawaswali, wanafunga tu mwezi wa Ramadhaan. Nimeshawaamrisha Swalah zaidi ya mara moja. Mmoja wao aliswali siku kadhaa, na pindi niliporejea Misri nikitoka Saudi Arabia nikakuta ameacha Swalah. Na (mke) wa pili anasema hajui kitu katika Qur-aan hata al-Faatihah. Nifanye nini?

Jibu: Ni juu yako uwafanye watubu na uwabainishie umuhimu wa Swalah na kwamba ndio nguzo ya Uislamu na kwamba kuiacha ni kufuru, wakitubu Alhamdulillaah ubaki nao. Na ikiwa hawakutubu, ni wajibu kwako kutengana nao na Allaah Atakupa walio bora kuliko wao:

“Mwenye kuacha kitu kwa ajili ya Allaah, Allaah Humpa kilicho bora kuliko hicho.”

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) Anasema:

وَمَن يَتَّقِ اللَّـهَ يَجْعَل لَّهُ مَخْرَجًا وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لَا يَحْتَسِبُ

“Na yeyote (yule) anayemcha Allaah Atamajaalia njia (ya kutoka katika matatizo). Na Atamruzuku kutoka njia ambayo hatizamii.” (65:02-03) Na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) Anasema: وَمَن يَتَّقِ اللَّـهَ يَجْعَل لَّهُ مِنْ أَمْرِهِ يُسْرًا “Na yeyote (yule) anayemcha Allaah Atamjaalia wepesi katika jambo lake.” (65:04)

Ni wajibu kwako uwafunze, uwafunze al-Faatihah na Suurah fupi katika nyakati ambazo nyoyo zitakuwa zimetulia, uwafunze na ujitahidi kwa hilo na wewe utakuwa mwenye ujira mkubwa. Wakishindwa kusoma al-Faatihah, walete badala yake Adhkaar; kwa kusema “Subhaanallaah”,”Alhamdulillaah”, “Laa ilaaha illa Allaah”, “Allaahu Akbar” na “Laa Hawlah wa laa Quwwatah illa billaah”. Mtume (´alayhis-Salaam) kaamrisha asiyeweza al-Faatihah alete Dhikr hizi. Akishindwa, alete Dhikr hizi. Lakini iwe ni pamoja na kujaribu katika nyakati za mbele kuihifadhi (al-Faatihah) na kujifunza nayo.

Muulizaji: Kuwafanya kwake watubu ni kwa ajili ya kuacha kwao Swalah? Na ikiwa hawakutubu, ni juu yake kufarakana nao?

Ibn Baaz: Ndio.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Nuur ´alaad-Darb (770)
  • Imechapishwa: 10/03/2018