Swali: Wagonjwa wengi wanapuuza swalah na wanasema kuwa watalipa swalah watakapopona na baadhi ya wengine wanasema ni vipi wataswali ilihali hawawezi kujitwahirisha na wala hawawezi kujinasua kutokamana na najisi. Kip mnawanasihi watu hawa?

Jibu: Maradhi hayamzuii mtu kuswali kwa hoja ya kushindwa kujitwahirisha muda wa kuwa akili bado ipo. Bali ni lazima kwa mgonjwa kuswali kwa kiasi cha uwezo wake na ajitwahirishe kwa maji akiweza kufanya hivo. Asipoweza kutumia maji basi atafanya Tayammum na kuswali. Ni lazima kwake kuosha najisi kutoka mwilini mwake na kwenye nguo zake kipindi cha kuswali au abadilishe nguo najisi kwa nguo safi wakati wa kuswali. Akishindwa kuosha najisi na kubadilisha nguo najisi kwa nguo safi, basi litadondoka kwake jambo hilo na ataswali kulingana na hali yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ

”Mcheni Allaah muwezavyo.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Ninapokuamrisheni jambo, basi liendeeni kiasi na muwezavyo.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Alisema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia ´Imraan bin Huswayn (Radhiya Allaahu ´anh) wakati alipomshtakia maradhi ambapo akasema:

”Swali kwa kusimama. Usipoweza, kwa kukaa. Usipoweza, lalia bavu.”

Ameipokea al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” yake. an-Nasaa´iy ameipokea kwa cheni ya wapokezi Swahiyh na akazidisha:

“Asipoweza, basi kwa kuegemea.”

[1] 64:16

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/307)
  • Imechapishwa: 15/08/2022