Waalimu kuwabeba ndani ya gari wanafunzi wa viongozi wa masomo

Swali: Ni ipi hukumu ya yale yanayofanywa na baadhi ya wafanyakazi ambapo wanawabeba watoto wa mameneja wao na viongozi wao kuwapelekea majumbani mwao baada ya watoto wao kutoka masomoni. Wanafanya hivo ima kwa amri ya mameneja hao, kwa malipo au pasi na malipo, mmoja au wengi.

Jibu: Hili linafanana na kumpa zawadi mfanyakazi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kupitia yale yaliyopokelewa na Imaam Ahmad:

“Kumpa zawadi mfanyakazi ni kukhini.”

Khiyana ni haramu. Amesema (Ta´ala):

وَمَا كَانَ لِنَبِيٍّ أَن يَغُلَّ ۚ وَمَن يَغْلُلْ يَأْتِ بِمَا غَلَّ يَوْمَ الْقِيَامَةِ

“Haimpasi Mtume yeyote kukhini [ngawira] na yeyote atakayekhini basi atakuja na kile alichokikhini siku ya Qiyaamah.” (03:161)

Ikiwa mtu huyu anawabeba watoto wa kiume au watoto wa kike wa mudiri kwenda masomoni na anawarudisha nyumbani, hili bila ya shaka ni zawadi. Ikiwa ni kwa malipo, basi hapo kunakuja kitu kingine: hilo linamshughulisha na kazi yake rasmi. Kwa sababu kuwapeleka watoto na kuwarudisha kutoka masomoni kunakuwa katika wakati wa kazi yake rasmi. Haijuzu kabisa kwa mudiri au mkuu wa chuo kuwatumia wale walioko chini yake katika kazi ambayo ni maalum kwake. Akifanya hivo basi anaidhulumu nchi na kama anawalazimisha basi anawadhulumu vilevile wafanyakazi hawa. Baadhi ya watu mfanyakazi asipofanya kile anachotaka basi anamfanyia madhara mfanyakazi huyu. Akiwa na kumhamisha sehemu nyingine anafanya hivo au kumnyima haki ambayo ni wajibu wake basi anafanya hivo. Haya ni haramu.

Ni wajibu kwetu kumcha Allaah (´Azza wa Jall). Tutambue kuwa tutakutana na Allaah na tutambue kuwa tutafufuliwa hali ya kuwa miguu peku, uchi na pasi na kutahiriwa. Kwa hivyo si halali kwa yeyote kumdhulumu mwingine katika wale ambao Allaah amewafanya wakawa chini ya mikono yake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (60) http://binothaimeen.net/content/1363
  • Imechapishwa: 26/11/2019