Vipi swawm ya mzazi ambaye damu yake imerudi ndani ya masiku arubaini?


Swali: Mwanamke mwenye damu ya uzazi akisafika ndani ya wiki halafu akafunga pamoja na waislamu wenzake katika Ramadhaan masiku maalum ambapo baadaye damu yake ikarudi tena, je, anatakiwa kuacha kufunga katika hali hii? Je, ni lazima kwake kulipa masiku aliyofunga na masiku ambapo aliacha kufunga?

Jibu: Mwanamke mwenye damu ya uzazi akisafika ndani ya masiku arubaini ambapo akafunga kisha damu yake ikarudi tena ndani ya masiku haya arubaini, basi swawm yake ni sahihi. Ni wajibu kwake kuacha kuswali na kufunga katika yale masiku ambayo damu itakuwa imerudi. Kwa sababu ni mwenye kutokwa na damu ya uzazi mpaka pale ataposafika au akakamilisha masiku arubaini. Pindi atapotimiza masiku arubaini basi ni wajibu kwake kuoga ijapokuwa hatoona kusafika. Kwa sababu siku arubaini ndio kikomo cha nifasi kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanachuoni. Baada ya hapo ni wajibu kwake kutawadha wakati wa muda wa kila swalah mpaka pale damu yake itapokatika kabisa. Hivyo ndivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivomwamrisha mwanamke mwenye kutokwa na damu ya ugonjwa. Mume wake ana haki ya kustarehe naye baada ya masiku arubaini ijapokuwa atakuwa bado hajaona kusafika. Kwa sababu damu na hali ni kama alivosema ni damu ya ugonjwa isiyomzuia kuswali, kufunga wala haimzuii mume kustarehe na mke wake. Lakini baada ya masiku arubaini damu yake ikikutana na ada yake ya hedhi basi atatakiwa kuacha swalah, swawm na kuiizingatia kuwa ni hedhi.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (15/198-199)
  • Imechapishwa: 23/05/2018