Vipi swawm ya ambaye ametokwa na madhiy kwa kutazama filamu chafu?


Swali: Mtu akibusu ilihali amefunga au akatazama baadhi ya filamu za uchi ambapo akatokwa na madhiy alipe swawm yake? Ikiwa hayo aliyafanya katika masiku mbalimbali kafara inakuwa kwa kufululiza au siku mbalimbali?

Jibu: Kutokwa na madhiy hakuharibu swawm kutokana na maoni sahihi zaidi ya wanachuoni. Ni mamoja yametoka kwa kumbusu mke, kutazama baadhi ya filamu au kitu kingine kinachoamsha matamanio. Lakini hata hivyo haijuzu kwa muislamu kutazama filamu za uchi wala kusikiliza yale aliyoharamisha Allaah katika muziki na ala za muziki. Ama kuhusu kutokwa na manii kwa matamanio ndio kunaharibu swawm. Ni mamoja yametoka kwa kukumbatia, kubusu, kutazama kwa kukariri au sababu nyingine inayoamsha matamanio kama vile punyeto na mengineyo. Kuhusu kuota au kufikiria hakuharibu swawm ijapokuwa mtu atatokwa na manii kwa sababu ya mawili hayo.

Si lazima kulipa kwa kufululiza katika kulipa deni la Ramadhaan. Inafaa kwa mtu kulipa masiku tofauti kutokana na kuenea kwa maneno Yake (Ta´ala):

فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۚ

”Yule atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu au akawa safarini, basi akamilishe idadi katika masiku mengineyo.” (02:184)

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (15/267-268)
  • Imechapishwa: 27/05/2018