Vichinjwa Vya ISIS


Imebainika kuwa ISIS ni wajinga. Hawafahamu wala hawaelewi Dini. Kuna ndugu amenieleza ya kwamba kuna mtu mmoja mwenye fikira za ISIS amenieleza kwa nini wanawakata watu viungo vya mwili na kuwachinja kama kondoo. Hawawakati kwa upanga. Wanawachinja kwa kisu. Wanasema wanatendea kazi Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati aliposema kuwaambia makafiri wa Quraysh:

“Nimekuja kwenu kwa uchinjaji.”

Wanasema kuwa wanatendea kazi Hadiyth hii. Tafsiri ya Hadiyth hii ni maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nimeamrishwa kuwapiga watu vita mpaka washuhudie ya kwamba hapana mola mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah.”

Maana ya uchinjaji ni kuwapiga vita washirikina. Isitoshe Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakupigana vita na washirikina kwa njia wanayoifanya. Alipigana vita na washirikina na akawaamrisha kutomuua mtu dhaifu, mzee, mwanamke wala mtoto. Ama kuhusu watu hawa, wanakusudia kuwaua Waislamu. Hawamrehemu mtu dhaifu, mzee, mtoto wala mwanamke. Wameeneza ufisadi kati ya watu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakukusudia hilo. Vipi hiyo ndio itakuwa maana ilihali Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mimi si jengine isipokuwa ni neema yenye kuongoza.”?

Allaah (´Azza wa Jalla) Amesema:

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِّلْعَالَمِينَ

“Na Hatukukutuma isipokuwa uwe ni Rahmah kwa walimwengu.” (21:107)

Vipi basi mtu anaweza kusema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikusudia hili? Hili linaonesha dalili tosha ya ujinga wao uliobobea. Ni wajinga.

Wanadai kuwa wanataka kusimamisha ukhaliyfah wa Kiislamu kwa kufanya uasi kwa mtawala, kwa kuwaua Waislamu, kwa kumwaga damu, kwa kuharibu na kuipa Uislamu sura mbaya. Vipi itakuweje? Vipi kutasimamishwa ukhaliyfah wa Uislamu kwa kwenda kinyume na Uislamu? Asiyekuwa na kitu hawezi pia kupeana kitu. Ni nani aliyekwambia ni wajibu kwako wewe kusimamisha ukhaliyfah wa Uislamu? Hakuna yeyote katika Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah aliyesema hivi. Sio wajibu kwa Muislamu yeyote kwa dhati yake kusimamisha ukhaliyfah wa Kiislamu. Hili linafanywa na mtawala.

  • Mhusika: Shaykh Muhammad bin ´Umar Baazmuul
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.sahab.net/forums/index.php?showtopic=146687
  • Imechapishwa: 06/11/2016