Swali: Nitumie njia gani kujua ni nani natakiwa kukaa chini yake na kama ana utata au fikra zilizopinda?

Jibu: Waulizeni wale watu walio na uzowefu juu yake. Vilevile tazama maneno, vitendo na wakati huo huo uwaulize wale wanaomjua. Kuhusu mtu ambaye hajulikani na wewe pia hujui lolote juu yake usimwandame mpaka pale utapohakikisha kwanza elimu, dini na anavyoitendea kazi elimu yake. Baadhi ya Salaf wanasema:

“Hakika elimu hii ni dini. Hivyo basi, tazama ni kutoka kwa kina nani mnaichukua dini yenu.”

Usichukue elimu kutoka kwa kila mtu. Anza kwanza kutazama. Utapokuwa na uhakika juu yake ndio sasa uchukue elimu kutoka kwake. Haya khaswa khaswa hii leo ambapo wajinga na wanaojidai wana elimu wamekuwa wengi ilihali uhalisia wa mambo hawana elimu yoyote. Matokeo yake wao wenyewe wanapotea na wanawapoteza wengine. Hivi ndivyo alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Pili wanaolingania katika maovu wamekuwa wengi. Allaah asiwafanye kuwa wengi! Leo ni wajibu kwa mwanafunzi achukue tahadhari zaidi na kuthibitisha mambo ni kutoka kwa kina nani ambao anataka kuchukua elimu kutoka kwao.

Mwalimu akiwa anafunza sehemu ya hadharani akikosea atadhihiri. Tatizo liko kwa yule anayefunza sehemu ya siri na isiyojulikana. Hapa ndio kuna tatizo. Tahadharini na sehemu za kujificha!

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Furqaan (07) http://alfawzan.af.org.sa/node/2050
  • Imechapishwa: 26/12/2016