Swali: Ni ipi hukumu ya mwenye kumpwekesha Allaah (Ta´ala) lakini hata hivyo anafanya uvivu kufanya baadhi ya ´ibaadah?

Jibu: Anakuwa na imani pungufu. Kadhalika mwenye kufanya baadhi ya maasi imani yake inapungua kwa mtazamo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Kwa sababu wanaona kuwa imani ni maneno, matendo na kuamini. Inapanda kwa utiifu na inashuka kwa maasi. Katika mfano wa hayo ni kuacha kufunga Ramadhaan bila udhuru au baadhi ya siku zake. Hii ni dhambi kubwa inayoshukisha imani na kuidhoofisha. Baadhi ya wanachuoni wanamkufurisha kwa kitendo hicho. Lakini maoni sahihi ni kwamba hakufuru kwa kitendo hicho midhali anakubali kuwa ni wajibu. Hapo ni pale ambapo ataacha kufunga baadhi ya siku kwa sababu ya kuchukulia wepesi na uzembe. Vivyo hivyo akichelewesha kulipa zakaah ndani ya wakati wake au akaacha kutoa kabisa ni dhambi na udhaifu katika imani. Baadhi ya wanachuoni wanaona kuwa ni kafiri kwa kuacha kwake kuitoa. Kadhalika akiwakata ndugu zake au akawaasi wazazi wake ni jambo linaloshukisha imani na kuifanya ikawa dhaifu. Vivyo hivyo maasi mengine yote.

Kuhusu kuacha swalah ni jambo linalopingana na imani na linawajibisha kuritadi ijapokuwa mtu hakupinga uwajibu wake kwa mujibu wa maoni yenye nguvu zaidi ya wanachuoni. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kichwa cha mambo ni Uislamu, nguzo yake ni swalah, kilele chake ni Jihaad katika njia ya Allaah.”

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ahadi iliopo kati yetu na wao ni swalah. Hivyo basi, yule mwenye kuiacha amekufuru.”

Zipo Hadiyth zengine vilvilevile zinavyothibitisha hilo.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (01/55) https://binbaz.org.sa/fatwas/866/%D8%A7%D9%84%D8%AA%D8%B9%D8%B2%D9%8A%D8%A9-%D9%81%D9%8A-%D8%A7%D9%87%D9%84-%D8%A7%D9%84%D9%85%D8%B9%D8%A7%D8%B5%D9%8A
  • Imechapishwa: 14/12/2019