Utumiaji mbaya wa matashi ya Allaah

Swali: Nimewasikia baadhi ya watu wakisema kwamba ukifanya kitendo chochote cha kidini kama vile kuswali, kufunga au kingine chochote cha kidunia na ukaulizwa juu yake kama umeswali au umefunga basi usijibu kwa kusema (إن شاء الله) ”Allaah akitaka”. Badala yake unatakiwa kusema ”ndio” kwa sababu umekwishakifanya. Unasemaje juu ya hilo?

Jibu: Hili linahitajia upambanuzi. Ama katika mambo ya ´ibaadah ni sawa ukasema ”Nimeswali – Allaah akitaka, nimefunga – Allaah akitaka”. Kwa sababu hajui kama amekamilisha na imekubaliwa kutoka kwake. Hapo kale waumini walikuwa wakifanya Istithnaa´ katika imani na funga zao. Kwa sababu hawajui kama zimekamilika au hazikukamilika. Mmoja wao alikuwa anaweza kusema ”Nimefunga – Allaah akitaka, mimi ni muumini – Allaah akitaka”.

Kuhusu mambo ambayo hakuna haja ya kuweka matashi ya Allaah ni kama mfano pindi unaposema ”nililala – Allaah akitaka”. Hapa huhitajii kusema hivi. Mfano mwingine ”Nilikula chakula cha asubuhi au cha jioni – Allaah akitaka”. Hapa huhitajii kuweka neno ”Allaah akitaka.” Kwa sababu mambo haya hayahitajii matashi wakati wa kuyaelezea. Kwa sababu ni mambo ya kawaida na isitoshe amekwishayafanya na yakamalizika. Hilo ni tofauti na mambo ya ´ibaadah ambayo hajui kama ameyakamilisha au amepunguza haki yake. Akisema ”Allaah akitaka” basi ni kwa ajili ya kutafuta baraka kwa jina Lake (Subhaanahu wa Ta´ala) na kutahadhari kutokamana na kudai jambo ambalo pengine hakulikamilisha na kutekeleza haki yake.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (05/403)
  • Imechapishwa: 08/12/2020