´Uthmaan bin Madh´uun (Radhiya Allaahu ´anh)


Alikuwa anaitwa ´Uthmaan bin Madh´uun bin Habiyb bin Wahb bin Hudhaafah bin Jumah bin ´Amr bin Husways bin Ka´b al-Jumhiy, Abus-Saa-ib.

Alikuwa ni miongoni mwa wakuu wa Muhaajiruun na miongoni mwa mawalii wa Allaah wenye kumcha ambaye alifuzu kwa kufa kipindi cha uhai wa Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawaswalia swalah ya jeneza. Abus-Saa-ib alikuwa wa kwanza kuzikwa al-Baqiy´.

Sa´iyd bin al-Musayyab amesema:

“Nilimsikia Sa´d akisema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumwacha ´Uthmaan bin Madh´uun kuishi maisha ya utawa. Vinginevyo na sisi tungefanya hivo.”[1]

Ibn ´Abdil-Barr amesema:

Alikuwa miongoni mwa wale watu waliojiepusha na pombe kabla ya kuja Uislamu.

´Uthmaan bin Madh´uun amesema:

“Sinywi kinywaji kinachoiondosha akili yangu, nikachekwa na yule ambaye ni duni kabisa kuliko mimi na hali ikanipelekea kumuoa Mahram yangu.”

Khabari hii ni yenye kukatika na haikuthibiti. Pombe iliharamishwa baada ya kufa kwake.

Ibn ´Abdil-Barr amesema:

“Abus-Saa-ib aliingia katika Uislamu akiwa ni mtu wa 14. Alifanya Hijrah mara mbili. Alifariki baada ya vita vya Badr. Alikuwa ni mfanya ´ibaadah mwenye bidii. Yeye, ´Aliy na Abu Dharr walitaka kuishi maisha ya utawa.”[2]

Abu Ishaaq as-Saa-ib ameeleza kwamba Abu Burdah amesema:

“Mke wa ´Uthmaan bin Madh´uun aliingia nyumbani kwa wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wakamuona yuko katika hali isiyokuwa nzuri wakasema: “Una nini? Hakuna katika Quraysh ambaye ni tajiri zaidi kuliko mume wako?” Ndipo akasema: “Nyusiku zake ni mwenye kusimama kuswali na michana yake ni mwenye kufunga. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokutana naye akamwambia: “Hivi wewe huna kiigizo chema kwangu?” Baada ya hapo akawaendea hali ya kuwa amejitia manukato kama kwamba ni biharusi.”[3]

Alifariki katika Sha´baan mwaka wa 03.

al-Qaasim bin Muhammad ameeleza kupitia kwa ´Aaishah ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimbusu ´Uthmaan bin Madh´uun baada ya kufa. Machozi yake yalikuwa yakitiririka kwenye mashavu ya ´Uthmaan bin Madh´uun.”

Swahiyh kwa mujibu wa at-Tirmidhiy.

Umm-ul-´Alaa´, mmoja katika wale wanawake waliokula kiapo cha usikivu na utiifu, ametaja namna ambavo ´Uthmaan bin Madh´uun aliwalalamikia ubaya wa hali yake. Hakukupita muda mrefu mpaka akapatwa na ugonjwa mpaka akafa. Wakati alipokuja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nikasema: “ Nakushuhudia, ee Abus-Saa-ib, kwamba Allaah amekukirimu.” Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ni kipi kimekujuza?” Nikasema: “Sijui. Ni nani?” Akasema: “Yeye amekwishakufa. Naapa kwa Allaah kwamba hakika mimi namtarajia kheri. Mimi ni Mtume wa Allaah lakini sijui ni kipi atakachofanywa.” ´Aaishah akasema: “Naapa kwa Allaah kwamba sintomsifu baada yake mwingine yeyote.” Kisha akasema: “Jambo hilo likanihuzunisha. Nikalala na nikaota kwamba ´Uthmaan yuko na chemchem inayotiririka. Nikamwaleza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akasema: “Hayo ni matendo yake.”[4]

[1] al-Bukhaariy (5073).

[2] al-Isti´aab (8/62).

[3] Ibn Sa´d (3/1/287).

[4] al-Bukhaariy (3929).

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Siyar A´laam-in-Nubalaa' (1/161-162)
  • Imechapishwa: 19/01/2021