Utathubutu vipi kumpongeza kafiri?

Waja wa Allaah mcheni Allaah (´Azza wa Jall) na tambueni kuwa haijuzu kuwapongeza wakristo kwa sikukuu zao. Ni vipi mnawapa hongera wakristo na muislamu akamwambia kafiri:

“Nakutakia sikukuu yenye furaha.”

ilihali Allaah (´Azza wa Jall) amempa matishio kafiri huyu ya kudumu Motoni milele akifa juu ya ukafiri wake? Imaam Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema katika kitabu chake kitukufu “Ahkaam Ahl-idh-Dhimmah” ambapo amesema:

“Kuwapongeza kwa nembo za kikafiri ambazo ni maalum kwao ni jambo la haramu kwa maafikiano. Kwa mfano kuwapongeza kwa sikukuu zao na funga zao kwa kusema: “Nakutakia sikukuu yenye furaha” au “Nakupongeza kwa sikukuu hii” na mfano wake. Kitendo hichi, mwenye nacho akisalimika na ukafiri, basi ni miongoni mwa mambo ya haramu. Ni jambo ambalo liko katika kiwango cha kuwapongeza kwa kusujudia kwake msalaba. Bali kitendo hicho [cha pongezi] ni dhambi kubwa mbele ya Allaah na cha hasira zaidi mbele Yake kuliko kumpongeza kwa kunywa pombe, kuiua nafsi, kuizini tupu ya haramu na mfano wake.

Anayempongeza mja kwa maasi, uzushi au ukafiri basi amejipelekea mwenyewe katika hasira na ghadhabu za Allaah.”

Miongoni mwa yale yaliyothibitishwa pia na wanachuoni wetu wa leo ni yale yaliyosemwa na Shaykh Ibn ´Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) ambapo amesema:

“Kuhusu kuwapongeza kwa sikukuu – sikukuu za wakristo na makafiri wengine – ni kitendo cha haramu pasi na shaka. Pengine muislamu asilisamike kutokamana na kufuru. Kwa sababu kupongezana kwa sikukuu za ukafiri ni kuziridhia. Kuridhia ukafiri ni ukafiri. Miongoni mwa hayo ni kuwapongeza kwa yale yanayoitwa “sikukuu ya krismasi” au “sikukuu ya pasaka” na sikukuu nyenginezo mfano wa hizo. Sikukuu kama hizi hazijuzu kabisa. Haijalishi kitu hata kama wao wanatupongeza kwa sikukuu zetu. Sisi hatuwapongezi kwa sikukuu zao. Tofauti ni kwamba wao kutupongeza kwa sikukuu zetu ni upongezaji ambao ni haki. Ama sisi kuwapongeza wao kwa sikukuu zao ni upongezaji ambao ni batili.”

Miongoni mwa aina za kusherehekea sikukuu zao ni yale yanayofanywa na waislamu wengi pale wanaponunua yale yanayohusiana na sikukuu hii na mwaka mpya katika miti, picha au rangi zinazofahamisha juu ya sikukuu yao. Kadhalika yale yanayofanywa na baadhi yao pale wanaporusha fataki za moto unapoingia mwaka mpya nusu ya usiku. Hakika utashangaa kuona mfano wa matendo kama haya yakifanywa na waislamu wa leo, jambo ambalo linafahamisha udhaifu wa dini na udhaifu wa Tawhiyd.

  • Mhusika: Shaykh Khaalid bin Dhwahwiy adh-Dhwafayriy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://aldhafiri.net/?audio=%D8%AD%D8%B1%D9%85%D8%A9-%D9%85%D9%88%D8%A7%D9%84%D8%A7%D8%A9-%D8%A7%D9%84%D9%8A%D9%87%D9%88%D8%AF-%D9%88%D8%A7%D9%84%D9%86%D8%B5%D8%A7%D8%B1%D9%89-%D9%88-%D8%AA%D9%87%D9%86%D8%A6%D8%AA%D9%87%D9%85
  • Imechapishwa: 16/12/2019