Utangulizi wa al-Fawzaan juu ya kitabu cha Shaykh Rabiy´ al-Madkhaliy “Manhaj-ul-Anbiyaa´”

Pale ilipokuwa jambo la makundi haya mbalimbali yanautia Uislamu khatarini na jengine ni kwamba linaweza kuwazuia wale wanaotaka kuingia katika Uislamu ndipo ikawa ni wajibu kuyabainisha na kubainisha kuwa hayana lolote kuhusiana na Uislamu. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ الَّذِينَ فَرَّقُوا دِينَهُمْ وَكَانُوا شِيَعًا لَّسْتَ مِنْهُمْ فِي شَيْءٍ

“Hakika wale waliofarakisha dini yao na wakawa makundi makundi, huna lolote kuhusiana na wao.” (06:159)

Jengine ni kuwa Uislamu unalingania katika kukusanyika juu ya haki. Amesema (Ta´ala):

وَمَا وَصَّيْنَا بِهِ إِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ وَعِيسَىٰ ۖ أَنْ أَقِيمُوا الدِّينَ وَلَا تَتَفَرَّقُوا فِيهِ

“Tuliyomuusia kwayo Ibraahiym na Muusa na ‘Iysaa: Simamisheni dini na wala msifarikiane humo.” (42:13)

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا

“Shikamaneni nyote kwa pamoja na kamba ya Allaah na wala msifarikiane.” (03:103)

Pindi ilipokuwa kubainisha na kufichua hayo ni wajibu ndipo wakasimama baadhi ya wanachuoni walio na ghera na kuhakiki mambo ili kuzindua makosa ya makundi hayo na kubainisha namna wanavyoenda kinyume na mfumo wa Mitume pindi wanapolingania katika dini ya Allaah. Wamefanya hivo pengine wakarudi katika usawa. Haki ni kitu kilichompotea muumini. Lengo lingine la wao kufanya hivo ni ili wasidanganyike wengine na yale makosa wanayofuata. Miongoni mwa wanachuoni hao waliobeba kazi hii kubwa kwa kutendea kazi maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Dini ni kupeana nasaha. Dini ni kupeana nasaha. Dini ni kupeana nasaha.” Tukasema: “Kwa nani, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Kwa ajili ya Allaah, Kitabu Chake, Mtume Wake, viongozi wa waislamu na waislamu wa kawaida.””

Miongoni mwa wanachuoni hao waliobainisha na wakawatakia kheri wengine ni muheshimiwa, Shaykh na daktari Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy katika kitabu hichi kilichoko mbele yetu kikiwa na kichwa cha khabari “Manhaj-ul-Anbiyaa´ fiyd-Da´wah ilaa Allaah fiyhi al-Hikmah wal-´Aql”. Amebainisha – Allaah amuwafikishe na amjaze kheri – mfumo wa Mitume wanapolingania katika dini ya Allaah kwa mujibu wa ilivyokuja katika Qur-aan na Sunnah. Sambamba na hilo amelinganisha mfumo huo na mifumo ya makundi mengine yanayoenda kinyume ili kuonekane wazi tofauti kati ya mfumo wa Mitume na mifumo mingine hiyo mbalimbali inayoenda kinyume na mfumo wa Mitume. Ameijadili mifumo hiyo kwa mjadala wa kielimu na wa kiuadilifu ikitiliwa nguvu na mifano na dalili. Kitabu chake – na himdi zote anastahiki Allaah – kimeyafikia malengo. Ni chenye kutosheleza kwa yule anayeitaka haki na ni hoja dhidi ya mwenye kufanya ukaidi na jeuri. Tunamuomba Allaah amlipe thawabu juu ya kazi yake na anufaishe kwacho.

Swalah na salaam zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah wake.

Imeandikwa na:

Swaalih bin Fawzaan

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manhaj-ul-Anbiyaa´ fiyd-Da´wah ilaa Allaah fiyhi al-Hikmah wal-´Aql, uk. 25-26
  • Imechapishwa: 20/11/2016