Unawapendekezea Vijana Kusoma Vitabu Vya Sayyid Qutwub?


Swali: Je, unawapendekezea vijana kusoma vitabu vya Sayyid Qutwub? Unasemaje kuhusu vitabu vya Shaykh Rabiy´ juu ya Sayyid Qutwub kwa kuzingatia ya kwamba kuna ambao wanatahadharisha navyo?

Jibu: Sayyid Qutwub anazingatiwa kuwa ni mwandishi. Aliishi maisha ya kikafiri kwa miaka kumi na moja. Kisha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) akamwongoza. Hakukaa na wanachuoni. Alikuwa akizitegemea fikira zake. Kwa hiyo anazingatiwa kuwa ni mwandishi katika waandishi. Yeye na watu mfano wake wanaingia katika maneno ya Allaah (´Azza wa Jalla):

وَالشُّعَرَاءُ يَتَّبِعُهُمُ الْغَاوُونَ أَلَمْ تَرَ أَنَّهُمْ فِي كُلِّ وَادٍ يَهِيمُونَ وَأَنَّهُمْ يَقُولُونَ مَا لَا يَفْعَلُونَ إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَذَكَرُوا اللَّـهَ كَثِيرًا وَانتَصَرُوا مِن بَعْدِ مَا ظُلِمُوا ۗ وَسَيَعْلَمُ الَّذِينَ ظَلَمُوا أَيَّ مُنقَلَبٍ يَنقَلِبُونَ

“Washairi wanafuatwa na wapotofu. Je, huoni kwamba wao katika kila bonde wanatangatanga? Nao wanasema yale wasiyoyafanya – isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema na wakamtaja Allaah kwa wingi na wakapata nusura baada ya kudhulumiwa. [Na hivi karibuni] watakuja kujua wale waliodhulumu mgeuko gani watakaogeuka.” (26:224-227)

Mimi namuuliza muulizaji: Je, wewe umekwishasoma Tafsiyr ya Ibn Kathiyr yote? Umesoma ”as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy yote? Umesoma ”as-Swahiyh” ya Muslim yote? Umesoma ”al-Musnad” ya Ahmad yote? Umesoma ”as-Sunan” ya Abu Daawuud yote? Umesoma ”al-Jaamiy´” ya at-Tirmidhiy yote? Umesoma ”as-Sunan” ya an-Nasaa´iy yote kabla ya kuanza kusoma vitabu vya Sayyid Qutwub?

Baadhi ya watu wamekuwa Takfiyriyyuun baada ya kuanza kusoma vitabu vya Sayyid Qutwub kwa sababa mara nyingi anatumia neno ”Twaaghuut”. Hata na mimi natumia neno ”Twaaghuut”, lakini mara nyingi simaanishi kuwa Twaaghuut huyu ni kafiri. Kwa ajili hiyo mimi sipendekezi kusoma vitabu vya Sayyid Qutwub, vitabu vya Muhammad al-Ghazaaliy, vitabu vya Muhammad Qutwub wala vitabu vya Zaynab al-Ghazaaliy.

Ndugu! Someni vitabu vya Sunnah kama ”Kitaab-ut-Tawhiyd” cha Ibn Khuzaymah, ”as-Sunnah” cha Ibn Abiy ´Aaswim, ”ash-Shariy´ah” cha al-Aajurriy, ”Sharh Usuul I´tiqaad Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah” cha al-Laalakaa´iy. Someni vitabu vya Sunnah kama ”as-Sunnah” cha Muhammad bin Naswr al-Marwaziy, ”al-Iymaah” cha al-Qaasim bin Sallaam na vitabu vya wanachuoni wengine wa kale. Allaah ameihifadhi dini Yake:

إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ

”Hakika Sisi ndio tumeteremsha Ukumbusho na hakika Sisi bila shaka ndio Wenye kuihifadhi.” (15:09)

Simkafirishi Sayyid Qutwub. Lakini nasema kuwa mtu asisome vitabu vyake.

Allaah amjaze kheri nyingi ndugu yetu Rabiy´ bin Haadiy (Hafidhwahu Allaah). Ametoa nasaha na kubainisha upindaji na upotevu uliyomo kwenye vitabu vya Sayyid Qutwub.

  • Mhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://muqbel.net/sounds.php?sound_id=15
  • Imechapishwa: 08/04/2017