Ni jambo lisilokuwa na shaka mlipuliko wa leo Kuwait unaenda kinyume na Qur-aan, Sunnah na mfumo wa Salaf na maandiko mengine yote ya Kishari´ah. Si dini, akili wala maumbile haiyakubali matendo haya machafu. Kitendo kama hichi kinatoka kwa mtu ambaye fikira zake na maumbile yake yamechafuliwa na fikira za Khawaarij na zisizokuwa za sawa. Wamesafishwa vichwa na hivyo wakaona haki kuwa ni batili na batili kuwa ni haki. Hatushangazwi na matendo kama haya. Ni ya tangu hapo kale. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kumuua Mu´aahad[1] basi hatonusa harufu ya Pepo. Harufu yake inapatikana miaka arobaini.”[2]

Hili linahusiana na yule mwenye kumuua Mu´aahad. Mu´aahad ni yule kafiri mwenye kuishi katika mji wa Kiislamu au ameingia kwa mujibu wa masharti ya waislamu. Haijuzu kumuua. Haijuzu kumhadaa. Haijuzu kukiuka dhimma ya mtawala. Ni watawala ndio wanaotakiwa kushughulikia yale makosa yanayofanywa na watu ndani ya nchi. Wao ndio wana haki ya kuwasimamishia adhabu. Sio mtu ni mtu. Na sio vijana na wapumbavu.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameisifu aina hii ya watu katika Hadiyth nyingi. Yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakutahadharisha pote lolote au kundi lenye kuwatia waislamu katika khatari kubwa kama hawa Khawaarij. Wana majina na ngozi mbali mbali, lakini wote ni wenye kukubaliana juu ya kuwafanyia uasi waislamu. Baadhi yao wanaitwa ISIS, wengine al-Qaa´idah, wengine an-Nusrah, wengine Qutbiyyah, wengine Takfiyryyuun na wengineo. Wote wana fikira za khatari za Khawaarij za Takfiyr. Fikiria ya kwamba kiongozi wa Khawaarij hawa aitwae Dhul-Khuwaysirah hakuwa radhi na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati alipokuwa akigawa mateka siku ya Hunayn. Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni mwenye kugawa kwa uadilifu na hamdhulumu yeyote. Mtu huyu akaja na kufoka:

“Ee Muhammad! Fanya uadilifu! Hakika hukufanya uadilifu!”

Ikiwa hawakuwa radhi na hukumu ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni vipi watakuwa radhi na sisi na kwa watawala wetu wa Kiislamu? Alisema:

“Ee Muhammad! Fanya uadilifu! Hakika hukufanya uadilifu!” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Ole wako! Nani atakayefanya uadilifu ikiwa mimi sikufanya uadilifu?”

Wakati yule mtu alipotoka pale ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamuashiria na kusema:

“Kupitia aina ya mtu huyu watajitokeza watu; mtazidharau swalah zenu kutokana na swalah zao, swawm zenu kutokana na swawm zao, kisomo chenu kutokana na kisomo chao.”

Bi maana udhahiri wao ni ucha Mungu na wema. Kiasi cha kwamba Maswahabah wanazidharau ´ibaadah zao walipokuwa wakiona ´ibaadah za watu hawa. Haya yanasemwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ili tusije kudanganyika na udhahiri wa watu hawa pale wanapozifanyia kazi hukumu, adhabu na Uislamu – Uislamu hauna lolote na wao. Kisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Wanasoma Qur-aan pasi na kuvuka koo zao.”

Haifiki kwenye mioyo. Hawaitendei kazi. Hawaiwakilishi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wanatoka katika dini kama jinsi mshale unavyotoka kwenye upinde.”

Bi maana wanatoka katika Uislamu kama jinsi mshale unavyotoka kwenye upinda wake; wakati mshale unapotoka kwenye upinde wake hupati athari yake yoyote. Hawana lolote kuhusiana na Uislamu. Ndio maana wanachuoni wengi wanaonelea kuwa Khawaarij sio waislamu; wanaonelea kuwa ni makafiri. Wanachuoni wengine wanaonelea kuwa ni waislamu pamoja na kuwa ni kipote potofu, kilichopinda na cha khatari.

Hawakuwa radhi na ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) ambapo wakawa wamemuua nyumbani kwake. Wakaizunguka nyumba yake, wakamuua na kumchapa mke wake. Hawakuwa radhi na ´Aliy, ´Amr bin al-´Aasw na Mu´aawiyah (Radhiya Allaahu ´anhum).

Tazama hila na uchafu wao! Usiku mmoja katika Ramadhaan watatu katika wao walikutana katika Msikiti Mtakatifu wakipanga kuwaua makhaliyfah na viongozi. Mmoja wao anapanga kumuua ´Aliy. Mwingine anapanga kumuua Mu´aawiyah. Mwingine anapanga kumuua ´Amr bin al-´Aasw (Radhiya Allaahu ´anhum) – kwenye Ka´bah! Huku ndio kunaitwa “kusafishwa kichwa”. Maumbile yao yamekuwa kichwa chini miguu juu. Muuaji wa ´Aliy akafanikiwa na wale wawili wengine wakafeli. Lakini hata hivyo wote katika usiku mmoja wakakubaliana juu ya kitendo hichi cha unyama dhidi ya watu wabora kabisa walioko katika ardhi; Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Walipomkamata Swahabah ´Abdullaah bin Khabbaab (Radhiya Allaahu ´anh) na mwanamke wake mjamzito wakipita kwenye kiganja cha mti wa mtende. Chini ya kiganja cha mti wa mtende huu mmoja wao akapata tende na kuila. Mwenzake akamwambia:

“Unachukua kisichokuwa halali kwako?”

Tazama maumbile haya kichwa chini miguu juu! Wanamshambulia Swahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na eti wanaogopa kula tende moja. Wakati mmoja wao alipotaka kuua nguruwe mwenzake akamwambia:

“Huenda ukaua nguruwe ya mtu anayelipa Jizyah.”

Wakati huo huo wanawaua Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Baada ya hapo walimuua na wakapasua tumbo la mwanamke wake na kuua kipomoko. Haya ndio maumbile yao.

al-Bukhaariy ametaja katika”at-Taariykh al-Kabiyr” namna ambavyo Swahabah mmoja kwa jina ´Abdullaah bin Qurdh (Radhiya Allaahu ´anh) alipokuwa njiani anaelekea nyumbani ametoka katika Jihaad katika njia ya Allaah. Njiani akielekea Ahwaaz akataka kuswali. Alipofika kwenye msikiti akaona kuwa ni Khawaarij. Wakamwambia:

“Karibu, ewe adui wa Allaah!”

Wanamwambia hivyo Swahabah. Swahabah huyu ametoka vitani. Amesikia adhaana na anataka kuswali. Akawaambia: “Mimi ni Swahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Wakasema: “Tunaapa kwa Allaah tutakuua!” Akasema: “Mtaridhia kwangu kile ambacho Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliridhia kutoka kwangu?” Wakamuuliza: “Na ni kipi alichoridhia?” Akasema: “Nilikuja kwake hali ya kuwa ni kafiri na nikawa nimeshuhudia ya kwamba hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Akaukubali Uislamu wangu.” Wakasema: “Tunaapa kwa Allaah hatuukubali Uislamu wako. Wewe ni kafiri.” Baada ya hapo wakamuua (Radhiya Allaahu ´anh). Huyu alikuwa ni Swahabah ambaye alikuwa anaelekea nyumbani kwake ametoka vitani na anataka kuswali ambapo akawaeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliukubali Uislamu wake. Pamoja na haya hawakuridhia.

Huu ndio mtazama wao mweusi juu ya jamii. Ndio maana wanaziita kuwa ni “jamii za kipindi cha kikafiri”. Hawaonelei wewe, mtawala wako, wafanya kazi wako, polisi, maaskari wala wananchi wenye kuishi chini yake pasi na kumkataza na kutojiunga na wao kuwa ni waislamu. Wanatangamana nao kama makafiri. Hawaswali kwenye misikiti yao. Endapo watalazimika kufanya hivo na mmoja katika imamu ambaye sio katika wao akawaongoza katika swalah wanairudi. Kwa sababu wanaonelea kuwa wote hawa ni makafiri na sio waislamu.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametutahadharisha juu ya watu hawa katika Hadiyth nyingi. Ni wajibu kwetu kujua hukumu za Kishari´ah juu ya mambo haya. Ni wajibu kwetu kutambua kuwa watu hawa khatari yao ni kubwa juu ya Uislamu na waislamu. Asiwepo yeyote atakayehadaika nao kwa sababu wanaonesha kitu chenye kuafikiana na Uislamu. Uislamu ni wenye kujitenga mbali kabisa na watu hawa.

Vilevile tunatakiwa kutahadhari juu ya watoto zetu. Wanatangamna na nani? Wanatembea na nani? Wanasafiri na nani? Wengi wao wanatangamana na wale wenye kuitwa kuwa ni watu wa dini. Tahamaki unakuja kusikia wako katika miji ya fujo. Wanawapeleka wana wetu, vijana wetu na wajinga katika miji hiyo kwa kutumia jina la Jihaad katika njia ya Allaah wakati wao na watoto wao wamekaa majumbani mwao. Hawataki watoto wao waende huko. Bali wanaposikia watoto wao wanataka kwenda huko wanawasiliana na serikali kuwazuia. Wao wenyewe hawaendi huko. Ni lini tuliwahi kusikia viongozi hawa wapotevu wenye kuwashaji´isha vijana kwenda katika miji hiyo amejilipua? Wenye kujilipua tu na hawa vijana masikini waliodanganyika. Wanafikiri kuwa wako katika haki na wanaelekea katika njia ya Peponi wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wao ndio wauliwaji wabaya kabisa chini ya mbingu.”

Miongoni mwa fikira zao za khatari ni pamoja na yale tuliyosema kuwa Salaf na wanachuoni wametofautiana kama ni waislamu au sio waislamu. Hadiyth za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zenye kutahadharisha juu ya matendo yao ya kiunyama ni ushahidi tosha juu ya ubaya uliyoje wa hali za Khawaarij hawa.

[1] al-Bukhaariy (3166) na an-Nasaa’iy (4762).)

[2] Imaam Ibn-ul-Athiyr (Rahimahu Allaah) amesema:

“Mtu Mu´aahad ni yule ambaye kuna mkataba kati yako wewe na yeye. Mara nyingi waislamu walioahidiwa amana ndio huitwa hivyo. Vilevile makafiri wengine ni wenye kuitwa hivyo ikiwa kuna mkataba wa amani wa muda kati ya pande zote mbili.” (an-Nihaayah (2/275))

  • Mhusika: Shaykh Khaalid bin Dhwahwiy adh-Dhwufayriy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://ar.miraath.net/sites/default/files/audio/khutoorat_ul_khawarij_sh… Tarehe: 1436-09-09/2015-06-26
  • Imechapishwa: 07/11/2016