Unachotakiwa kufanya pindi imamu anapozidisha Rak´ah

Swali: Nimekusikia katika moja katika Khutbah za ijumaa ukisema kwamba ni wajibu kwa mswaliji asimfuate imamu pindi atapozidisha Rak´ah katika swalah yake ya faradhi kama kwa mfano akizidisha Rak´ah ya tano. Ni vipi mswaliji atamzindua imamu? Naomba kuwekewa wazi. Imamu asiporudi na akaendelea na swalah yake katika Rak´ah ya tano mswaliji afanye nini? Je, asimame kumfuata imamu au aendelee kukaa kwake chini?

Jibu: Kumzindua imamu ni jambo limebainishwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliposema:

“Wanaume wamsabihi Allaah na wanawake wapige makofi.”

Wanaume waseme:

سبحان الله

“Allaah ametakasika.”

Wakati fulani imamu anaposimama katika Rak´ah ya tano katika swalah yenye Rak´ah nne anaambiwa hivo lakini hata hivyo imamu huyu anaendelea. Katika hali hii mswaliji afanye nini? Maamuma akae chini na wala asimfuate imamu. Imamu atapoleta salamu ndipo nawe utoe salamu. Hilo ni kwa sababu baadhi ya imamu wanasimama katika Rak´ah ya tano kwa sababu wamesahau kusoma al-Faatihah katika Rak´ah moja wapo[1]. Wanaposahau kusoma al-Faatihah katika Rak´ah moja wapo Rak´ah ile inafutika na anasimama kuswali Rak´ah nyingine ichukue nafasi yake. Kwa hivyo matokeo yake wanasimama kuswali Rak´ah ya tano badala ya ile ya Rak´ah ambayo alisahau kusoma al-Faatihah. Kwa hiyo swalah ya imamu huyu inakuwa sio batili. Kwa sababu ameswali Rak´ah ya tano kwa sababu ya kukamilisha swalah yake ambayo imepungua kwa sababu ya kuacha nguzo miongoni mwa nguzo.

Ama tutapojua kuwa imamu amesimama katika Rak´ah ya tano au katika Rak´ah yoyote ya ziada, basi tunatakiwa kunuia kutengana naye na kutoa salamu kivyetu na kumwacha. Kwa mfano anaswali Fajr na tukatambua kuwa imamu amesoma al-Faatihah vilivyo, Rukuu´ kikamilifu, Sujuud kikamilifu, kuinuka kutoka katika Rukuu´ kikamilifu, kikao kamilifu na Tashahhud ya mwisho kikamilifu na tukajua kuwa amesoma ndani yake, tutapoyakinisha kuwa amesimama katika Rak´ah ya ziada basi hatumfuati. Badala yake tunakaa na kutoa salamu. Ama midhali hatuna yakini basi tunatakiwa kukaa chini. Lakini tunamsubiri ili tuweze kutoa salamu pamoja naye.

[1] Tazama https://firqatunnajia.com/imamu-anazidisha-rakah-ya-tano-kwa-sababu-alisahau-al-faatihah/

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (50) http://binothaimeen.net/content/1152
  • Imechapishwa: 26/06/2019