1Neno la Mwenyezi Mungu lilinijia: 2Wewe mtu! Mwambie mfalme wa Tiro kuwa mimi Bwana Mwenyezi Mungu nasema hivi: “Wewe una kiburi cha moyo na umesema kwamba wewe ni mungu, kwamba umekalia kiti cha enzi cha miungu, umekaa mbali huko baharini. Lakini, wewe ni binadamu tu wala si Mungu, ingawa wajiona kuwa una hekima kama Mungu. 3Haya! Wewe wajiona mwenye hekima kuliko Danieli, wadhani hakuna siri yoyote usiyoijua. 4Kwa hekima na akili yako umejipatia utajiri, umejikusanyia dhahabu na fedha ukaziweka katika hazina zako. 5Kwa busara yako kubwa katika biashara umejiongezea utajiri wako, ukawa na kiburi kwa mali zako! 6Kwa hiyo mimi Bwana Mwenyezi Mungu nasema hivi: Kwa vile unajiona mwenye hekima kama Mungu, 7basi nitakuletea watu wageni, mataifa katili kuliko yote. Wataharibu fahari ya hekima yako na kuchafua uzuri wako. 8Watakutumbukiza chini shimoni, nawe utakufa kifo cha kikatili kilindini mwa bahari. 9Je, utajiona bado kuwa mungu mbele ya hao watakaokuua? Mikononi mwa hao watakaokuangamiza,

 utatambua kuwa wewe ni mtu tu, wala si Mungu! 10Utakufa kifo cha aibu kubwa mikononi mwa watu wa mataifa. Ni mimi Bwana Mwenyezi Mungu nimesema.”

  • Marejeo: Ezekieli 28:01 https://www.bible.com/sw/bible/74/EZK.28.BHN
  • Imechapishwa: 31/01/2020