Swali: Umezungumzia umuhimu wa kulingania katika Tawhiyd na kusema ya kwamba ndio jambo la kwanza ambalo mtu anatakiwa kulingania kwalo kama jinsi ilivo katika Hadiyth ya Mu´aadh (Radhiya Allaahu ´anhu) wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipomtuma Yemen. Ee Shaykh! Mu´aadh alitumwa kwa makafiri na ndio maana akamwamrisha awalinganie katika Tawhiyd na sisi leo ni Waislamu na watu wako katika Uislamu. Hivyo basi, ni kwa nini mtu aanze nao Tawhiyd ilihali tayari wanaijua?

Jibu: Kafiri analinganiwa katika Tawhiyd kama jinsi Muislamu pia anafundishwa nayo kwa njia ya mafunzo. Muislamu anatakiwa kufunzwa ni nini Tawhiyd kwa sababu anaweza kuwa kwenye kitu katika shirki au Bid´ah na yeye hajui. Anatakiwa kuwekewa nayo wazi na kusomeshwa nayo.

Sisi tunawafunza watoto wetu na Waislamu Tawhiyd ili wasitumbukie kwenye kosa. Hawakukingwa na makosa. Ni lazima waijue Tawhiyd na vipengele vyake, shirki na vipengele vyake. Haitoshelezi kuwa ni Waislamu. Isitoshe, hawawezi kuwa Waislamu isipokuwa kwa Tawhiyd. Anaweza kuwa anajinasibisha na Uislamu ilihali ni mshirikina, anaabudu kaburi, anawategemea majini, mashaytwaan, mawalii na watu wema. Pamoja na yote hayo akasema kuwa ni Muislamu. Uhakika wa mambo kwa hali hii sio Muislamu. Sio kila anayesema kuwa ni Muislamu anakuwa ni Muislamu kweli.

Ukiongezea juu ya hilo, hata yule Muislamu mwenye I´tiqaad sahihi yuko khatarini. Ni lazima abainishiwe Tawhiyd na aina zake, shirki na aina zake ili aweze kujiepusha na shirki na awe na uimara kwenye Tawhiyd.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-is-Saffaariniyyah (02) http://www.alfawzan.af.org.sa/sites/default/files/sfranih_02.mp3
  • Imechapishwa: 01/07/2018