Umeuliza na kujibiwa – lakini mbona bado uko na wasiwasi?

Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

27- an-Nawwaas bin Sam’aan (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“… na dhambi ni ile inayoyumbayumba [ulio na mashaka nayo] katika nafsi yako na hupendelei watu waitambue ijapokuwa watu wamekupa shauri lao la Kishari´ah [kukupendelea nacho].”

Mtu anaweza kwenda kwa Muftiy na akamuuliza swali juu ya jambo na Muftiy akamwambia kuwa suala hilo ni la sawa. Lakini hata hivyo wakati huo huo ndani ya moyo wake kukabaki mashaka. Muftiy yeye anatoa fatwa kulingana na yanayomdhihirikia katika swali. Muulizaji huenda akawa na mambo ambayo hakuyaweka wazi au hakuweza kuyaweka wazi inavyopaswa. Katika hali hii anabaki hali ya kuwa yeye ndiye mwenye kuihukumu nafsi yake na uwajibu wa ´ibaadah umefungamanishwa na yeye na kupewa thawabu na adhabu kumefungamanishwa kwake yeye. Ndani ya moyo wake kukibaki mashaka na asipate utulivu, basi ashikamane na kile anachohisi ndani ya nafsi yake kwa njia ya kujiepusha na mambo yenye kutia shaka na yanayoyumbayumba katika nafsi yake.

  • Mhusika: Shaykh Swaalih bin ´Abdil-´Aziyz Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Arba´iyn an-Nawawiyyah, uk. 373
  • Imechapishwa: 17/05/2020