Swali: Katika amana ni kuhukumu kwa Shari´ah. Lakini tunaishi katika nchi isiyohukumu kwa Shari´ah ya Allaah na zinazotumika ni kanuni za Uingereza na Ufaransa. Kipi kinachotupasa katika nchi yetu? Tuna uwajibu gani ya kuwatii watawala hawa? Tutangamane nao vipi?

Jibu: Ambaye anaishi katika nchi inayohukumu kwa kanuni zilizotungwa – ni mamoja kanuni hizo ni za kifaransa, kingereza, kimarekani au kwenginepo – ni lazima kwake ashirikiane na wengine juu ya wema na kumcha Allaah na awanasihi wale ambao Allaah amewatawalishia jambo lao. Anatakiwa atoe nasaha za pamoja kwa njia nzuri ambayo itawaathiri wale wasimamizi na awalinganie kusikiliza mawaidha na ukumbusho. Asifanye hivo kwa mabavu ambayo yatasababisha kuchukuliwa hatua wale wenye kumcha Allaah na kufungwa jela. Lakini anatakiwa atoe nasaha kwa maneno mazuri, njia nzuri na ushirikiano mpaka Allaah ajaalie faraja na njia ya kutokea.

Ni lazima kwa waislamu kushirikiana juu ya wema na kumcha Allaah, watoe nasaha kwa ajili ya Allaah, walinganie kwa Allaah kwa hekima na maneno mazuri. Waislamu wanatakiwa kuwaandikia watawala kwa njia endelevu mara kwa mara, wawasiliane nao kupitia wale watu wao mashuhuri na wakuu wao kwa lengo la kuwanasihi na kuwataka wahukumu kwa Shari´ah. Pindi wananchi watakuwa wakweli, wakajitahidi katika jambo hilo na wakawasiliana na watawala, basi Allaah atajaalia faraja na njia ya kutokea.

Kuhusu yale yanayofanywa na baadhi ya watu ambapo wanafanya mauaji ya kuvizia na kumwaga damu ni mambo yasiyosaidia kitu. Kinyume chake yanawadhuru waislamu na kudhuru ulinganizi. Matokeo yake waislamu wanabaki katika madhara makubwa na kulazimiana na majumba yao au kufungwa jela, kitu ambacho kinadhuru ulinganizi na hakiisaidii. Aidha kinawadhuru waislamu na hakiwasaidii. Kinachowanufaisha ni kusaidiana juu ya wema na kumcha Allaah, kuwanasihi waislamu, kufanya duara za kielimu ndani ya misikiti na kwenginepo. Kulingania kwa Allaah miongoni mwa askari na kati ya tabaka mbalimbali za jamii na kuwasiliana na watawala na kuwanasihi kwa njia nzuri na maneno mazuri. Kufanya hivo ndio kuko karibu zaidi na kheri na mbali zaidi na kuwekwa gerezani na madhara mengine.

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/4260/بم-ينصح-المقيمون-ببلاد-لا-تحكم-بالشريعة
  • Imechapishwa: 14/06/2022