Malaika sio maana kama wanavosema[1]. Bali Malaika ni wenye viwiliwili na maumbo. Wana uwezo wa kujibadilisha kwa maumbo mbalimbali Allaah amewapa uwezo wa kufanya hivo. Kwa ajili hii Jibriyl (´alayhis-Salaam) alikuwa akimjia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika umbile la bwana mmoja. Allaah amewapa uwezo wa kuweza kujibadilisha katika maumbile mbalimbali kwa ajili ya manufaa ya mwanadamu. Kwa sababu mwanadamu hawezi kustahamili kuwaona Malaika katika umbile ambalo Allaah amewaumba kwalo. Walikuwa wanamjia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika umbile la bwana mmoja kwa ajili ya kumfanyia urafiki mwanadamu. Hawaonekani katika umbile lao na uhakika wao isipokuwa wakati wa adhabu. Amesema (Ta´ala):

يَوْمَ يَرَوْنَ الْمَلَائِكَةَ لَا بُشْرَىٰ يَوْمَئِذٍ لِّلْمُجْرِمِينَ

“Siku watakayowaona Malaika hakutakuwa na bishara njema Siku hiyo kwa wahalifu.”[2]

Vilevile wakati wa kifo mtu huwaona. Kipindi hicho humuona Malaika wa mauti. Lakini duniani na kipindi ambacho mtu bado anaishi hawaoni. Kwa sababu hana uwezo wa kuwaona.

Allaah amewaumba kutokana na nuru. Amewaumba mashaytwaan kutokana na moto, hivo ndivo ilivyotajwa katika Qur-aan. Amemuumba Aadam kutokana na udongo. Allaah juu ya kila jambo ni muweza.

Makafiri wanaamini kuwa Malaika ni wasichana wa Allaah. Amesema (Ta´ala):

وَجَعَلُوا الْمَلَائِكَةَ الَّذِينَ هُمْ عِبَادُ الرَّحْمَـٰنِ إِنَاثًا ۚ أَشَهِدُوا خَلْقَهُمْ ۚ سَتُكْتَبُ شَهَادَتُهُمْ وَيُسْأَلُونَ

“Wakawafanya Malaika, ambao ni waja wa Mwingi wa huruma, kuwa ni wa kike. Je, kwani wameshuhudia uumbaji wao?  Hakika utaandikwa ushahidi wao na wataulizwa.”[3]

[1] Muhammad ´Abduh na Muhammad Rashiyd Ridhwaa.

[2] 25:22

[3] 43:19

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 211-213
  • Imechapishwa: 15/03/2020