Uislamu utakuwa juu ulimwenguni kote

87- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Uislamu utayoyoma kama mifumo kwenye kitambaa mpaka pale ambapo swawm, swalah, taratibu za ´ibaadah wala zakaah havitotambulika tena. Katika usiku mmoja Kitabu cha Allaah (´Azza wa Jall) kitanyanyuliwa na juu ya ardhi hakutobaki hata Aayah moja. Kutabaki kundi la watu. Wazee wa kiume na wa kike watasema: ”Tuliwakuta baba zetu wakitamka neno hili ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` na sisi tunalisema.”[1]

al-Haakim ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye, na mambo ni kama alivosema.

Katika Hadiyth kuna khabari ya khatari inayosema kwamba ipo siku ambayo atari ya Uislamu itaondoka na Qur-aan itanyanyuliwa; hakutobaki ndani yake Aayah hata moja. Lakini hayo hayatotokea isipokuwa ni baada ya Uislamu kushinda na uwe juu ya ulimwenguni kote. Hayo yamesemwa na Allaah (Tabaarak wa Ta´ala):

هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ

“Yeye ndiye ambaye kamtuma Mtume Wake kwa uongofu na dini ya haki ili aishindishe juu ya dini zote japo watachukia washirikina.”[2]

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameyabainisha hayo katika Hadiyth nyingi ambapo baadhi zimeshatangulia kutajwa.

[1] Ibn Maajah (4049), al-Haakim (4/473) na Nu´aym bin Hammaad katika ”al-Fitan” (1/173 – asili).

[2] 09:33

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah (1/1/173)
  • Imechapishwa: 24/05/2019