Ni wajibu kwa walinganizi kutilia umuhimu jambo hili, kuwatahadharisha watu, kuwabainisha watu na kuwalingania katika Tawhiyd. Ni lazima kwao kuwafikishia dini hii watu na kuwawekea wazi watu ´Aqiydah kwa njia ya sawa na ya wazi. Huu ndio ufumbuzi. Yule anayetaka kutatua matatizo ya waislamu basi atambue kuwa huu ndio ufumbuzi. Inatosha kwa mtu mmoja tu ambaye atasimama kidete hali ya kumtakasia nia Allaah ambapo Allaah aokoe Ummah na vizazi vya watu. Hayo yametokea kupitia mikononi mwa walinganizi wenye Ikhlaasw na mtu mmojammoja.

Leo kuna makundi ya watu wanaolingania. Kuna rasilimali kubwa, pesa na mengine mengi. Lakini mtunda yako wapi? Lau angelikuwepo tu mlinganizi mmoja ambaye analingania kwa Allaah juu ya mfumo sahihi basi kungelikuwa manufaa makubwa. Hii leo walinganizi, makundi ya watu na mitandao imekuwa mingi. Lakini yako wapi matunda? Natija iko wapi? Bali shari inaongezeka tu. Shirki inazidi kuenea. Hayo yanatokana na kwamba makundi mengi katika haya hayakujengeka juu ya msingi sahihi. Vinginevyo mtu mmoja tu ambaye amesimama kidete kwa ajili ya Allaah anayefuata msingi sahihi na mfumo uliosalimika anawashinda walinganizi elfumoja, hayo yanatambulika kupitia wale walinganizi wenye Ikhlaasw walioshi hapo kabla.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 580
  • Imechapishwa: 04/09/2019