Uchafuchafu na umanjano havizingatiwi midhali damu ya hedhi imeshakauka


Swali: Mimi ni mwanamke ambaye najitahidi mara nyingi kuhusiana na suala la twahara. Lakini mara nyingi sioni weupe na hivyo muda ambao napata hedhi unarefuka kwa wiki mbili. Lakini hata hivyo damu naiona kwa muda wa siku saba tu; kunaweza kupungua au kuzidi siku moja. Baada ya hapo kunatoka vitu vikiwa na uchafu-uchafu, kisha baada ya hapo umanjano, halafu naona rutuba zinazomtoka mwanamke katika siku za kawaida. Kama nilivyosema mara nyingi sioni weupe. Naomba uniwekee wazi juu ya jambo hili. Ni lini mwanamke anajisafisha kutokamana na hedhi katika hali kama hii?

Jibu: Damu ya hedhi inapokatika na ikafuatiwa na uchafu au umanjano, havizingatiwi. Kwa msemo mwingine ni kwamba uchafu na umanjano havizingatiwi baada ya kuwa damu imeshakatika. Allaah (Ta´ala) amesema:

 وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْمَحِيضِ ۖ قُلْ هُوَ أَذًى

“Wanakuuliza kuhusu hedhi. Sema: “Hiyo ni dhara.”[1]

Dhara ni damu. Umm ´Atwiyyah amesema:

“Tulikuwa hatuzingatii umanjano na uchafu kuwa ni kitu.”

Hivi ndivyo ulivyo upokezi wa al-Bukhaariy. Upokezi wa Abu Daawuud umesema:

“Tulikuwa hatuzingatii umanjano na uchafu baada ya kutwaharika kuwa ni kitu.”[2]

 Pindi damu inakatika kusafika kumeshapatikana.

Kujengea juu ya hili tunamwambia mwanamke huyu midhali anaona damu ya hedhi kwa muda wa siku saba, kisha ikafuatiwa na uchafu au umanjano, basi anatakiwa aoge maadamu damu ya hedhi imeshakatika baada ya kutimiza siku saba. Halafu baada ya hapo aswali, afunge na aingiliwe na mume wake – ikiwa yuko na mume – haijalishi kitu hata kama atakuwa na uchafu na umanjano.

[1] 02:222

[2] Abu Daawuud (307).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa' ash-Shahriy (36) http://binothaimeen.net/content/805
  • Imechapishwa: 18/03/2018