Swali: Kuna mkusanyiko wa maswali yanayozungukia juu ya Hijaab. Baadhi ya maswali hayo yanabainisha namna ya Hijaab iliopo kwa baadhi ya wanawake katika mahospitali hizi. Tunamwomba atubainishie sifa ya Hijaab inayokubalika katika Shari´ah ambayo ni ya lazima.

Jibu: Hijaab inayokubalika katika Shari´ah ni mwanamke kufunika mwili wake mzima mbele ya wanamme ikiwa ni pamoja na kichwa, kifua, miguu na nyayo. Mwili mzima wa mwanamke hautakiwi kuonekana mbele ya wanamme wasiokuwa Mahram zake. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَإِذَا سَأَلْتُمُوهُنَّ مَتَاعًا فَاسْأَلُوهُنَّ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ ۚ ذَٰلِكُمْ أَطْهَرُ لِقُلُوبِكُمْ وَقُلُوبِهِنَّ

“Mnapowauliza [wake zake] haja yoyote, basi waulizeni nyuma ya pazia. Hivyo ni utwaharifu zaidi kwa nyoyo zenu na nyoyo zao.”[1]

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا

“Ee Nabii! Waambie wake zako na mabinti zako – na wanawake [wote] wa Waumini – ya kwamba [nje ya nyumbani] wajiteremshie mavazi yao ya juu; hivyo kunapeleka karibu zaidi watambulikane [kuwa ni wanawake wa heshima] na wasiudhiwe. Na Allaah ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.”[2]

Uso ndio pambo kubwa, vivyo hivyo nywele na mikono. Mwanamke anaweza kufunika uso wake kwa Niqaab ambayo ni ile inayoonyesha macho mawili au jicho moja na uso unakuwa umefunikwa. Anahitajia kuacha wazi macho yake ili aweze kuona njia. Pia anaweza kujifunika kwa kitu kisichokuwa Niqaab kama mfano wa Khimaar isiyomzuia kuona njia. Lakini hata hivyo anatakiwa kuficha mapambo yake, afunike kichwa chake na mwili wake mzima.

Ni lazima kwa mwanamke kujiepusha kutumia mafuta yenye harufu wakati anapotoka kwenda sokoni, msikitini au kazini kama ni mwajiriwa.

[1] 33:53

[2] 24:31

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (06/24)
  • Imechapishwa: 17/02/2021