Abu Muhammad Twalhah bin ´Ubaydillaah bin ´Amr bin Ka´b bin Sa´d bin Taym bin Murrah bin Ka´b bin Lu-ayy bin Ghaalib bin Fihr bin Maalik bin an-Nadhwr bin Kinaanah al-Qurashiy at-Taymiy al-Makkiy.

Alikuwa ni mmoja katika wale kumi waliobashiriwa Pepo. Amepokea Hadiyth nyingi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Katika “al-Musnad” ya Baqiyy bin Makhlad ana Hadiyth 38.

Anazo Hadiyth mbili ambazo zimepokelewa na al-Bukhaariy na Muslim wote kwa pamoja. al-Bukhaariy amepokea kutoka kwake Hadiyth mbili peke yake na Muslim Hadiyth tatu.

Baadhi ya waliopokea kutoka kwake ni watoto wake Yahyaa, Muusa na ´Iysaa. Kadhalika as-Saa-ib bin Yaziyd, Maalik bin Aws bin al-Hadathaan, Abû ´Uthmaan an-Nahdiy, Qays bin Abiy Haazim, Maalik bin Abiy ´Aamir as-Aswbahiy, al-Ahnaf bin Qays at-Tamiymiy, Abu Salamah bin ´Abdir-Rahmaan na wengieno.

Muusa bin Twalhah amesema:

“Baba yangu alikuwa mweupe na mfupi kiasi. Alikuwa na kifua kipana na miguu mikubwa. Alikuwa na mabega mapana na pindi anapogeuka basi anageuza mwili mzima.”

Alikuwa miongoni mwa wale waliotangulia mwanzoni katika Uislamu. Akaudhiwa kwa ajili ya Allaah kisha akahajiri. Kuna maafikiano kwamba hakushiriki vita vya Badr kwa sababu ya safari ya kibiashara huko Shaam. Alisikitishwa juu ya kutoshiriki kwake.

Mkono wake ulipooza baada ya kumlinda kwao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika vita vya Uhud. Qays amesema:

“Niliona mkono wa Twalhah ambao amlimlinda kwao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika vita vya Uhud. Ulikuwa umepooza.” Ameipokea al-Bukhaariy.

Katika “as-Swahiyh” ya Muslim Abu Hurayrah amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa katika Hiraa´ pamoja na Abu Bakr, ´Umar, ´Uthmaan, ´Aliy, Twalhah na az-Zubayr. Tahamaki mlima ukaanza kutikisika. Ndipo Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Tulizana! Hakuna aliye juu yako isipokuwa Nabii, mkweli au shahidi.”[1]

Qabiyswah bin Jaabir amesema:

“Nilisuhubiana na Twalhah na sikumuona mtu anayepewa pesa nyingi pasi na yeye kuziomba kama anavopewa yeye.”

Su´daa bint ´Awf al-Murriyyah amesema:

“Siku moja nilimtembelea Twalhah na nikamkuta akiwa katika hali isiyokuwa ya uchangamfu. Nikamwambia: “Una nini? Pengine familia yako ndio imehuzunisha?” Akasema: “Hapana, naapa kwa Allaah. Wewe ni mke mzuri. Lakini nina pesa ambayo imekuwa nzito kwangu na kunihuzunisha.” Nikasema: “Kipi kimekutia uzito?” Akasema: “Waite watu wako.” Nikasema: “Ee kijana changu, waite watu wangu. Akagawanya pesa kati yao. Nikamuuliza muhifadhi hazina: “Kila mmoja amempa ngapi?” Akasema: “400000.””[2]

´Uthmaan bin ´Abdir-Rahmaan amesema:

“Twalhah bin ´Ubaydillaha alilipa deni la ´Ubaydullaah bin Ma´mar na ´Abdullaah bin ´Aamir bin Kurayzs ambalo lilikuwa ni dirhamu 80000.”

Qays amesema:

“Nilimuona Marwaan bin al-Hakam akimpiga Twalhah mshale kutoka kwenye upinde. Ukampata kwenye magoti yake na aliendelea kupata maumivu mpaka alipokufa.”

Qays amesema:

Ambaye alimuua Twalhah ni dhalimu kama yule ambaye alimuua ´Aliy.

ash-Sha´biy amesema:

“´Aliy alimuona Twalhah bondeni akiwa si mwenye uchangamfu. Akashuka chini, akampangusa mchanga usoni mwake na akasema: “Ee Abu Muhammad! Naona vibaya kukuona unauliwa kwenye mabonde chini ya mbingu. Namlalamikia Allaah masikitiko yangu nilionayo.”

Muhammad bin ´Abdillaah al-Answaariy:

“Mbashirie muuaji wa Twalhah kwamba ataingia Motoni.”

Maalik bin Abiy ´Aamir amesema:

“Alikuja bwana mmoja kwa Twalhah akasema: “Huyu myemeni – yaani Abu Hurayrah – ni mjuzi zaidi wa Hadiyth za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuliko nyinyi? Tunamsikia akisema mambo ambayo hatuyasikii kutoka kwenu.” Akasema: “Hakika ameyasikia mambo kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambayo sisi hatukuyasikia. Sisi tulikuwa ni wenye familia na tulikuwa tunamwendea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mida ya asubuhi na jioni. Upande wa pili yeye alikuwa ni masikini na hana mali yoyote. Daima alikuwa ni mwenye kusimama kwenye mlango wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa hivyo hatuna shaka kwamba ameyasikia ambayo sisi hatukuyasikia. Na hivi utampata mtu ambaye yuko na kheri akimnasibishia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kitu ambacho hakukisema?”[3]

Abu Habiybah, mtumwa aliyeachwa huru na Twalhah, amesema:

“Baada ya vita vya ngamia nilimtembelea ´Aliy nikiwa pamoja na ´Imraan bin Twalhah. Akamkaribisha na akamwambia asogee karibu naye. Kisha akasema: “Nataraji Allaah kunijaalia mimi na baba yako kuwa miongoni mwa wale ambao Allaah amesema juu yao:

وَنَزَعْنَا مَا فِي صُدُورِهِم مِّنْ غِلٍّ إِخْوَانًا عَلَىٰ سُرُرٍ مُّتَقَابِلِينَ

“Tutaondosha vifundo vya kinyongo vilivyomo vifuani mwao, hali ya kuwa ni ndugu, juu ya makochi yaliyoinuliwa wakikabiliana.”[4]

Wanamme wawili walioketi chini wakasema: “Allaah ni mwadilifu zaidi kuliko hivo wapigane jana na leo wawe ndugu Peponi.” Ndipo ´Aliy akasema: “Nyanyukeni na mwondoke. Mimi ni nani na Twalhah kama si ndugu? Ee mtoto wa ndugu yangu! Ukiwa na haja yoyote basi tujie.”

Yahyaa bin Bukayr, Khaliyfah bin Khayyaat na Abu Naswr al-Kalaabaadhiy wamesema:

“Ambaye alimuua Twalhah ni Marwaan bin al-Hakam.”

Twalhah alikuwa na watoto watukufu. Mbora wao alikuwa ni Muhammad as-Sajjaad. Alikuwa kijana, mbora na mfanya ´ibaadah. Alizaliwa katika uhai wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na yeye pia aliuliwa siku ya vita vya ngamia. ´Aliy akamuhuzunikia na akasema:

“Mapenzi yake kwa baba yake ndio yamemuua.”

[1] Muslim (2417) na at-Tirmidhiy (3698).

[2] al-Fasawiy katika ”al-Ma´rifah wat-Taariykh” (1/458), at-Twabaraaniy (195), Abu Nu´aym katika ”Hilyat-ul-Awliyaa’” (1/88) na Ibn Sa´d (3/1/157). al-Haythamiy amesema: ”Ameipokea at-Twabaraaniy na wanamme wake ni waaminifu.” (Majma´-uz-Zawaa-id (9/148)).

[3] at-Tirmidhiy (3834). Wanamme wake ni waaminifu na inazingatiwa ni nzuri kwa mujibu wa Ibn Hajar katika ”Fath-ul-Baariy”.

[4] 15:47

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (1/23-40)
  • Imechapishwa: 14/01/2021