Yahyaa bin Yahyaa at-Taymiy, Ja´far bin ´Abdillaah na kundi la wengine wamesema:

“Kuna mtu alikuja kwa Maalik bin Anas akasema: “Ee Abu ´Abdillaah:

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

“Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.”[1]

 “Yuko juu namna gani?”

Sijawahi kumuona Maalik anachukulia vibaya kama alivofanya siku hiyo. Akaanza kutokwa na jasho na wasikilizaji wakasubiri wamsikie atasema nini. Kisha akasema:

“Namna haifahamiki. Kuwa Kwake juu si kwamba hakufahamiki. Ni wajibu kuliamini hilo na kuuliza juu yake ni Bid´ah. Mimi nachelea wewe ni mpotevu.”

Kisha akaamrisha atolewe nje.

Haya yamethibiti kutoka kwa Maalik. Hii ndio ´Aqiydah ya Salaf. Hatufahamu namna Alivyo juu, ni kitu hatukijui kabisa. Kuwa Kwake juu kunajulikana, kama alivyotujuza katika Kitabu Chake, na ni kwa njia inayolinagana Naye. Hatuingii kwa undani katika jambo hilo na hatuleti uchambuzi, hatuingii katika malazimisho yanayopelekea katika hilo, si kwa kukanusha wala kwa kuthibitisha. Bali tunanyamaza na tunasimama pale waliposimama Salaf. Tutambue kuwa lau Kuwa juu kungelifasiriwa basi Maswahabah na Taabi´uun wangelikuwa wa mwanzo kufanya hivo. Midhali waliweza kukubali, wakalipitisha na kulinyamazia, tukajua kwa yakini kabisa kwamba Allaah (Jalla Jalaaluh) hawezi kufananishwa na yeyote katika sifa Zake, kustawa Kwake na kushuka Kwake. Ametakasika na kasoro na mapungufu kutokamana na yale wanayosema madhalimu.

[1] 20:05

  • Mhusika: Imam Shams-ud-Dîn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar-ul-´Uluww, uk. 141-142
  • Imechapishwa: 20/02/2019