Swali: Je, ibara hii ni sahihi:

“Tunashirikiana katika yale tunayoafikiana na tunapeana udhuru katika yale tunayotofautiana.”?

Jibu: Hii ni ibara inayokaririwa na baadhi ya walinganizi. Kwa mujibu wangu nawaona kuwa ni walinganizi wa Kiislamu wa jumla. Wanalingania katika Uislamu kwa jumla. Kuhusu walinganizi wanaolingania katika Qur-aan na Sunnah na kwa mfumo wa Salaf, mimi sijui kama kuna ambaye analingania katika Uislamu huu wa haki isipokuwa wale wanaojiita Ahl-ul-Hadiyth, Answaar-us-Sunanh au wafuasi wa Salaf. Kuhusu makundi mengine hayaweka hayo hadharani licha ya kuwa wanasema kuwa wako pamoja nasi katika kuifuata Qur-aan na Sunnah. Lakini ni neno wanalolitamka. Hawawezi kuyatendea kazi kwa kuwa masomo yao ya Shari´ah kwa mujibu wa Qur-aan na Sunanh ni kwa asilimia ndogo. Wanasema:

“Tunashirikiana katika yale tunayoafikiana na tunapeana udhuru katika yale tunayotofautiana.”

Maneno haya yana mtazamo kwa upande fulani. Sehemu ya kwanza ya sentesi iko wazi na haina neno: Tunashirikiana katika yale tunayoafikiana. Inayotakiwa kuangaliwa ni sehemu ya pili ya sentesi, nayo ni ile inayosema tunapeana udhuru katika yale tunayotofautiana. Ni ya sawa ikiwa tutaiweka katika mzani. Ina maana, tunapeana udhuru baada ya kupeana nasaha.

“Dini ni kupeana nasaha. Dini ni kupeana nasaha. Dini ni kupeana nasaha.” Tukasema: “Kwa nani, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Kwa Allaah, Mtume Wake, viongozi wa waislamu na watu wa kawaida.”[1]

Ikiwa tunaona sisi wenyewe ni wenye kutofautiana hata katika ule msingi wa Tawhiyd, ina maana ile Shahaadah, basi hatutakiwi kusameheana katika yale tunayotofautiana. Kinyume chake tunatakiwa kurejea katika Qur-aan na Sunnah na kukaribiana kiasi na tunavyoweza. Hapa hatuwezi kukubali tofauti, khaswa inapokuja katika mambo yanayohusiana na ´Aqiydah tofauti na mambo ya matawi. Ama kuyaacha mambo ya tofauti kama yalivyo na kusema tupeane udhuru katika mambo hayo na wakati huo huo hatujaribu kuimaliza tofauti hii kiasi na tunavyoweza, jambo hili linapingana na Aayah na Hadiyth zinazoamrisha umoja. Kitu kikubwa kinachotilia nguvu umoja ni kurejea katika Qur-aan na Sunnah. Amesema (Ta´ala):

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ

“Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamwamini Allaah na siku ya Mwisho.” (04:59)

Sisi tunajua wale wanaosema maneno haya wanaifanya tofauti ni jambo lililowekwa katika Shari´ah ambayo kwa mujibu wao ni jambo la lazima kuwepo. Sisi katika hili tunapingana nao kabisa na tunasema kuwa ni lazima kuhukumiana kwa Qur-aan na Sunnah. Endapo kutabaki kitu katika tofauti, basi haitakiwi iwe ni sababu ya kutofautiana na kutengana. Sisi khaswa katika nukta hii tuna ruwaza njema kwa Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Walikuwa wakisimama kwa haki. Walikuwa hata hawamnyamazii khaliyfah mwenyewe pindi anapokuwa amekosea katika maoni. Walikuwa wakimkataza. Lakini akiendelea kushikilia maoni yake, hawamfanyii uasi na wala hawaanzi kumjengea uadui. Kinyume chake wanakubaliana naye. Anawaamrisha kutoka kwenda katika Jihaad na wanatoka wote kwa pamoja kwa ajili ya kupigana katika njia ya Allaah, pamoja na kuwa bado wamebaki wametofautiana katika baadhi ya mambo.

[1] Muslim (55).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Juddah (34)
  • Imechapishwa: 12/02/2017