Swali: Kuna baadhi wamefanya safari na matembezi kuwa ni mfumo wa kuwalingania vijana ili wanyooke, waongoke na wahifadhi Qur-aan tukufu katika mizunguko ya kuhifadhi ya kila siku. Ni ipi hukumu ya kitendo hichi katika kulingania katika dini ya Allaah (´Azza wa Jall)?

Jibu: Kila kheri inapatikana kwa kuwafuata Salaf na kila shari inapatikana kwa kuzua waliokuja nyuma. Kujizoweza safari kama hizi na mfano wake ni katika njia za al-Ikhwaan al-Muslimuun na Ahl-ul-Bid´ah. Msikitini ndani yake kuna utulivu, Malaika wanateremka ndani yake, wakaaji wanafunikwa na rehema na Allaah anaibariki Da´wah inayofanywa misikitini ambayo Allaah ameamrisha ijengwe ili kuweze kutajwa ndani yake jina Lake, kumtukuza na kumuadhimisha. Katika hayo kunaingia vilevile kutafuta elimu ndani yake. Tusifanye mambo haya kama wanavyofanya Ahl-ul-Bid´ah wadh-Dhwalaal. Tukaeni misikitini na kujifunza kwa mfumo wa Salaf-us-Swaalih. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifunza msikitini. Historia ya Salaf inaonyesha kuwa walikuwa wakijifunza elimu misikitini na kulitokea wanachuoni vigogo na waliobobea kutoka katika misikiti. Safari hizi hazijatuletea wanafunzi sembuse wanachuoni vigogo na waliobobea. Narudi tena kusema kwamba kila kheri inapatikana kwa kuwafuata Salaf na kila shari inapatikana kwa kuzua waliokuja nyuma.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kashf-us-Sitaar, uk. 12
  • Imechapishwa: 30/10/2016