Kuhusiana na Allaah kuonekana Aakhirah ni miongoni mwa mambo makubwa na matukufu ya msingi wa dini. Watu wametofautiana kwayo katika madhehebu matano yanayojulikana:

1 – Madhehebu ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Hawa ni Maswahabah na wale wenye kuwafuata kwa wema ikiwa ni pamoja na maimamu. Wanaamini kuwa Allaah ataonekana Aakhirah kwa macho kabisa. Haya ndio madhehebu ya Maswahabah, Taabi´uun, maimamu na wenye kuwafuata, maimamu wa dini ikiwa ni pamoja na wale maimamu wane; Abu Haniyfah, Maalik, ash-Shaafi´iy, Ahmad, Sufyaan ath-Thawriy, Abu ´Amr al-Awzaa´iy, al-Layth bin Sa´d, Abu Yuusuf na wengineo katika maimamu na wanachuoni. Vilevile wanachuoni wengi wa Fiqh na Hadiyth wamo katika I´tiqaad hii. Kadhalika baadhi ya mapote ambayo yanajinasibisha na Hadiyth, kama Karraamiyyah na Saalimiyyah, wote wanathibitisha kuwa Allaah ataonekana Aakhirah kwa macho kabisa. Wao pia wanathibitisha kuwa Allaah ataonekana Aakhirah kwa macho kama ambavyo wanathibitisha pia kuwepo juu kwa Allaah, kwamba watamuona Mola Wao akiwa kwa juu. Wanathibitisha mambo mawili:

a) Wanathibitisha kuwepo juu kwa Allaah.

b) Wanathibitisha pia kuonekana kwa Allaah [Aakhirah].

2 – Madhehebu ya pili yamepinga kuwa Allaah ataonekana Aakhirah. Wanasema kuwa Allaah hatoonekana Aakhirah kwa macho na hana uwepo wa upande fulani wala mahala. Watu hawa wamepinga kuonekana kwa Allaah Aakhirah na kuwepo Kwake juu. Hawa ni madhehebu ya Jahmiyyah, Mu´tazilah, Khawaarij na Imaamiyyah. Imaamiyyah wana kauli mbili:

a) Wengi wao katika wale Imaamiyyah wa kale waliotangulia ambao ni Raafidhwah wanathibitisha kuonekana kwa Allaah Aakhirah.

b) Imaaamiyyah wengi katika waliokuja nyuma wanapinga kuwa Allaah ataonekana Aakhirah. Wameitwa Imaamiyyah kwa sababu wanaamini kuwepo kwa maimamu kumi na mbili. Watu hawa wanapinga mambo mawili; kuonekana kwa Allaah Aakhirah na kuwepo juu kwa Allaah. Wanasema kuwa Allaah hana mahala na hayuko juu ya viumbe. Badala yake yuko kila mahala.

3 – Madhehebu ya tatu ni madhehebu yalio kati ya Ahl-us-Sunnah na madhehebu ya Jahmiyyah. Wanasema kuwa Allaah ataonekana lakini bila ya kuwepo upande fulani. Wamethibitisha kuonekana na wakapinga uwepo Kwake kwa juu. Wamesema kuwa ataonekana lakini bila ya kuweko upande fulani. Haya ni madhehebu ya pote katika Kullaabiyyah na Ashaa´irah. Ni wenye kuyumbayumba kati ya hawa na hawa; kule kuthibitisha kwao kuonekana wakawa pamoja na Ahl-us-Sunnah na kukanusha kwao [kuonekana kwa upande wa] juu wakawa pamoja na Mu´tazilah.

Utaona siku zote madhehebu ya Ashaa´irah ni wenye kuyumbayumba baina ya hawa na hawa. Kwa ajili hii baadhi ya wanachuoni wameiwaita kuwa “watu wasiokuwa na jinsia”; si wasichana wala si wavulana.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (01/218-219)
  • Imechapishwa: 30/05/2020