Tofauti iliyopo juu ya neema na adhabu za kaburi

Kauli za wanachuoni kuhusiana na adhabu na neema za kaburi, nafsi na mwili ndio vinaadhibiwa au kimoja wapo? Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) aliulizwa juu ya masuala haya akajibu kuwa adhabu na neema inakuwa juu ya nafsi na mwili vyote viwili kwa maafikiano ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Nafsi inaneemeshwa na kuadhibiwa ikiwa ni yenye kutengana na mwili, na inaneemeshwa na kuadhibiwa ikiwa ni yenye mafungamano na mwili. Mwili unakuwa ni wenye mafungamano na nafsi na hivyo neema na adhabu katika hali hii inakuwa ni vitu viwili vyenye kukutana vyote kama jinsi moyo unakuwa ni wenye kutengana na mwili.

Adhabu na neema inakuwa kwenye kiwiliwili na si roho? Katika masuala haya kuna kauli tatu dhaifu na kauli tatu zisizokuwa dhaifu.

Kauli tatu za kwanza ambazo ni dhaifu ni zifuatazo:

Kauli ya kwanza: Neema na adhabu haiwi isipokuwa kwenye roho na mwili hauneemeshwi na wala hauadhibiwi kabisa. Hii ni kauli ya wanafalsafa ambao wanakanusha kuwa miili itarudishwa. Hawa ni makafiri kwa makubaliano ya waislamu.

Kauli ya pili: Kauli ya wenye kupinga kuadhibiwa kwa roho kabisa. Wanaonelea kuwa roho kipekee haineemeshwi na wala haiadhibiwi. Roho ni uhai. Haya yanasemwa na pote katika wanafalsafa miongoni mwa Mu´tazilah na Ash´ariyyah kama al-Qaadhwiy Abiy Bakr na wengine.

Kauli ya tatu: Maisha ya ndani ya kaburi hakuna neema wala adhabu. Hilo haliwi mpaka Qiyaamah kikubwa kisimame. Hii ni kauli ya baadhi ya Mu´tazilah na mfano wao. Kujengea juu ya kwamba roho haibaki baada ya kutengana na mwili na kwamba mwili hauneemeshwi na wala hauadhibiwi.

Ama wale wenye kuonelea kuwa ndani ya kaburi kuna adhabu na wanakubali Qiyaamah na wanathibitisha miili na roho kurudishwa wana kauli tatu:

Kauli ya kwanza: Neema na adhabu inakuwa kwenye roho tu. Wengi katika Mu´tazilah na wengineo katika wanafalsafa wanaonelea namna hii na ndio chaguo la Ibn Hazm na pote katika waislamu miongoni mwa Ahl-ul-Hadiyth na wanafalsafa.

Kauli ya pili: Neema na adhabu inakuwa kwenye roho na mwili vyote wivili.

Kauli ya tatu: Neema na adhabu inakuwa kwenye mwili peke yake.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (02/609-610)
  • Imechapishwa: 19/05/2020