Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

وَاسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ ۚ وَإِنَّهَا لَكَبِيرَةٌ إِلَّا عَلَى الْخَاشِعِينَ الَّذِينَ يَظُنُّونَ أَنَّهُم مُّلَاقُو رَبِّهِمْ وَأَنَّهُمْ إِلَيْهِ رَاجِعُونَ

“Tafuteni msaada kupitia subira na swalah, kwani hakika hilo ni kubwa isipokuwa kwa wanyenyekevu. Ambao wana yakini kwamba hakika wao watakutana na Mola wao na hakika wao Kwake ni wenye kurejea.”[1]

Allaah amewaamrisha kutaka msaada kwa mambo yao yote kupitia subira kwa aina zake zote. Nayo ni subira katika kumtii Allaah mpaka aitimize, subira ya kujizuia kumuasi Allaah mpaka ayaache na subira juu ya makadirio ya Allaah yenye kutia uchungu na asikasirike. Kufanya subira na kuizuia nafsi juu ya yale ambayo Allaah ameamrisha kuyafanyia subira kunapatikana msaada mkubwa juu ya kila jambo miongoni mwa mambo. Yule ambaye atafanya subira basi Allaah atamsubirisha.

Vivyo hivyo swalah ambayo ndio mzani wa imani na inamzuia mtu kutokamana na machafu na maovu. Mtu anatakiwa kutafuta msaada kupitia swalah katika mambo yote miongoni mwa mambo:

وَإِنَّهَا

“… kwani hakika hilo.”

Bi maana hiyo swalah.

لَكَبِيرَةٌ

“… ni kubwa… “

Bi maana jambo zito na gumu.

إِلَّا عَلَى الْخَاشِعِينَ

“… isipokuwa kwa wanyenyekevu.”

Kwao ni jambo rahisi na jepesi. Kwa sababu unyenyekevu, kumwogopa Allaah na kutaraji yale yaliyoko Kwake kunawapelekea kuitekeleza. Isitoshe swalah inawakunjulia vifua vyao kwa kule kutaraji thawabu zake na kuchelea adhabu Yake. Hili ni tofauti na yule asiyekuwa hivo. Hakuna kitu kinachomvutia kufanya hivo. Akiitekeleza basi inakuwa ni miongoni mwa mambo magumu zaidi kwake.

Kunyenyekea ni kule kunyenyekea, kutulizana, kuvunjika kwa moyo mbele ya Allaah hali ya kuwa ni wenye kujidhalilisha na kujidogesha, kumwamini Yeye na juu ya kukutana Naye. Ndio maana akasema:

الَّذِينَ يَظُنُّونَ أَنَّهُم مُّلَاقُو رَبِّهِمْ وَأَنَّهُمْ إِلَيْهِ رَاجِعُونَ

“Ambao wana yakini kwamba hakika wao watakutana na Mola wao na hakika wao Kwake ni wenye kurejea.”

Hivyo atawalipa kwa matendo yao. Haya ndio yamewafanyia wepesi ´ibaadah zao, kutulizana wakati wa mitihani na majanga na kuogopa kufanya maovu. Hawa ndio watapata neema yenye kudumu katika ghorofa zilizo juu kabisa.

Kuhusu yule asiyeamini kukutana na Mola wake basi swalah na ´ibaadah nyinginezo zinakuwa ni miongoni mwa mambo magumu zaidi kwake.

[1] 02:45-46

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-Kariym, uk. 42
  • Imechapishwa: 15/07/2020