Swawm haikubaliwi kwa mfungaji mpaka atoe Zakaat-ul-Fitwr?


Swali: Je, Hadiyth isemayo:

“Swawm ya Ramadhaan haipandishwi mpaka kutolewe Zakaat-ul-Fitwr.”

ni Swahiyh? Ikiwa muislamu aliyefunga na ambaye ni muhitaji hamiliki kile kiwango cha zakaah bado itakuwa ni wajibu kwake kutoa Zakaat-ul-Fitwr kutokana na usahihi wa Hadiyth au dalili zengine za Kishari´ah thabiti zilizosihi kutoka katika Sunnah?

Jibu: Zakaat-ul-Fitwr ni wajibu kwa kila muislamu ambaye anaweza kujikimu yeye mwenyewe midhali amemiliki chakula chake yeye na familia yake ile siku ya ´iyd na usiku wake. Kiwango chake ni Swaa´. Msingi wa hilo ni yale yaliyothibiti kutoka kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa):

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefaradhisha Zakaat-ul-Fitwr pishi ya tende au pishi ya ngano kwa muungwana na mtumwa, mvulana na msichana, mdogo na mkubwa katika waislamu. Ameamrisha itolewe kabla ya watu kutoka kwenda kuswali.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim na matamshi ni ya al-Bukhaariy.

Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) na yeye amepokea akisema:

“Tulikuwa wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tukitoa Swaa´ ya chakula. Kipindi hicho chakula chetu kilikuwa ni tende, shayiri, zabibu na jibini[2].”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Ni sawa kutoa chakula kinacholiwa katika mji kama mfano wa mchele na mfano wake.

Kiwango cha Swaa´ hapa ni ile Swaa´ ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni kukamatisha viganja vyote viwili [na kuvijaza] mara nne vya mwanaume ambaye ana umbile la wastani.

Mtu akiacha kutoa Zakaat-ul-Fitwr anapata dhambi na bado itakuwa ni wajibu kuitoa.

Kuhusu Hadiyth uliyoitaja hatujui usahihi wake.

[1] al-Bukhaariy (02/138-140), Muslim (02/677-678), Abu Daawuud (02/263-265), Maalik katika “al-Muwattwa´” (01/284), Ahmad (02/05) na wengineo.

[2] Tazama https://en.wikipedia.org/wiki/Cottage_cheese

  • Mhusika: al-Lajnah ad-Daaimah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa al-Lajnah ad-Daaimah (10/364-365)
  • Imechapishwa: 23/06/2017