Mu´aawiyah bin al-Hakam amesema:

“Nilikuwa na kondoo kati ya Uhud na al-Jawaaniyah wanaochungwa na kijakazi wangu. Siku moja akaja mbwa mwitu na akamchukua kondoo kutoka kwake. Mimi ni mwanaadamu wa kawaida ambaye hukasirika kama wanavyokasirika watu wengine. Nikaunyanyua mkono wangu na kumpiga kofi. Nikamwendea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumweleza yaliyopitika. Nikasikitika na kumwambia: “Ee Mtume wa Allaah! Si nimwache huru?” Akasema: “Mwite.”Nikamwita. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Allaah yuko wapi?” Akajibu: “Juu ya mbingu.” Akamuuliza: “Mimi ni nani?” Akajibu: “Wewe ni Mtume wa Allaah.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Mwache huru. Kwani hakika ni muumini.”[1]

 Hadiyth hii inatufidisha mambo mawili:

1- Inajuzu kumuulizia (Subhaanah) yuko wapi na kwamba inajuzu vilevile kujibu kwamba yuko juu ya mbingu.

2- Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwache huru. Kwani hakika ni muumini.”

Kuhusu swali la kwanza liko wazi. Swali linapelekea kwamba linafaa na kwamba inafaa vilevile kujibu kwamba yuko juu ya mbingu. Kwani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema:

“Allaah yuko wapi?”

Lau ingelikuwa haifai kuuliza hivo basi asingeliuliza. Mwanamke yule akamjibu kwamba yuko juu ya mbingu na akamkubalia juu ya hilo. Endapo ingelikuwa haijuzu kujibu kwamba Yeye (Subhanaah) yuko juu ya mbingu basi asingelimkubalia.

[1] Muslim (537), Abu Daawuud (930), an-Nasaa’iy (3/13), Maalik (2/776), Ibn Abiy ´Aaswim (479), al-Bayhaqiy, uk. 422, Ahmad (5/447) na Abu Daawuud at-Twayaalisiy (1105).

  • Mhusika: Imaam Abu Ya´laa Muhammad bin al-Husayn al-Farraa’
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ibtwaal-ut-Ta’wiyl (1/232)
  • Imechapishwa: 21/12/2018