Swali: Watu wa kijijini kwetu wana ada katika Ramadhaan ambayo ni kuswali vipindi vitano vya swalah; Dhurh, ´Aswr, Maghrib, ´Ishaa na Fajr. Wanafanya hivo ijumaa ya mwisho ya Ramadhaan. Wanaizingatiwa kuwa ni yenye kukidhi faradhi yoyote ambayo mtu hakuiswali au aliisahau. Ni ipi hukumu juu ya swalah hii? Je, ina msingi katika Shari´ah ya Uislamu?

Jibu: Hukumu juu ya swalah hii ni kwamba ni miongoni mwa Bid´ah. Haina msingi katika Shari´ah ya Uislamu. Haimzidishii mja mbele ya Mola Wake isipokuwa kumtenga mbali zaidi. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kila Bid´ah ni upotevu na kila upotevu ni Motoni.”

Bid´ah, ijapo wazushi wataifanya kuwa nzuri na wakaiona kuwa ni nzuri ndani ya nafsi zao, basi watambue kuwa ni mbaya mbele ya Allaah (´Azza wa Jall). Kwa sababu Mtume wao Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kila Bid´ah ni upotevu na kila upotevu ni Motoni.”

Vipindi hivi vitano vya swalah ambavo mtu anakidhi ijumaa ya mwisho ya Ramadhaan havina msingi wowote katika Shari´ah.

Jengine tunasema: je, wewe hukufanya kasoro isipokuwa katika swalah tano peke yake? Pengine umefanya kasoro siku nyingi na si katika swalah tano peke yake.

Muhimu ni kwamba zile swalah unazojua kuwa zimekupita basi unatakiwa kuzilipa pindi tu utapojua jambo hilo. Usicheleweshe. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule atakayepitiwa na usingizi kutokamana na swalah au akaisahau, basi aiswali atapokumbuka.”

Ama kitendo cha wewe kuswali swalah hizi tano, kwa ajili ya kuchukua tahadhari kutokana na madai yako, ni maovu na haifai.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb (104) http://binothaimeen.net/content/7906?q2=%D8%A7%D9%84%D8%B5%D9%84%D8%A7%D8%A9%20%D8%A2%D8%AE%D8%B1%20%D8%AC%D9%85%D8%B9%D8%A9%20%D9%85%D9%86%20%D8%B1%D9%85%D8%B6%D8%A7%D9%86%20%D9%82%D8%B6%D8%A7%D8%A1%20%D9%85%D8%A7%20%D9%81%D8%A7%D8%AA%D9%87%D9%85%20%D9%85%D9%86%20%D8%A7%D9%84%D9%81%D8%B1%D9%88%D8%B6
  • Imechapishwa: 21/05/2020