Ni lazima kuswali swalah ya ijumaa pasi na kujali imamu ni katika Ahl-us-Sunnah au Ahl-ul-Bid´ah au pasi na kujali ni mwema au mtenda dhambi. Haya yamesemwa na Ahmad. Imepokelewa kutoka kwa al-´Abbaas bin ´Abdil-´Adhwiym kwamba alimuuliza Abu ´Abdillaah [Ahmad bin Hanbal] kuhusu kuswali swalah ya ijumaa nyuma ya Mu´tazilah. Akasema:

“Mtu anatakiwa kushuhudia swalah ya ijumaa. Kama anajua kuwa swalah yake haisihi [kwa sababu ya ukafiri wao], basi atatakiwa kuirudi tena, na kama hajui kama ni sahihi au si sahihi, basi asiirudi upya.”

Ndipo nikamuuliza kwamba ikisemekana kuwa ameonelea kama walivoonelea. Akajibu:

“Mpaka awe na uhakika.”

Sijui kama kuna tofauti yoyote kwa wanachuoni juu ya hilo. Msingi wa hilo ni ueneaji wa maneno ya Allaah (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نُودِيَ لِلصَّلَاةِ مِن يَوْمِ الْجُمُعَةِ فَاسْعَوْا إِلَىٰ ذِكْرِ اللَّـهِ

”Enyi walioamini! Inaponadiwa kwa ajili ya swalah siku ya ijumaa, basi kimbilieni katika utajo wa Allaah.”[1]

Vivyo hivyo maafikiano ya Maswahabah. ´Abdullaah bin ´Umar na Maswahabah wengine wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa wakishuhudia swalah ya ijumaa pamoja na al-Hajjaaj na watu mfano wake. Haikupokelewa kutoka kwa mmoja katika wao kwamba alijitenga nao.

[1] 62:9

  • Mhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mughniy (3/169)
  • Imechapishwa: 29/01/2021