Hidmi zote ni stahiki ya Allaah, Mola wa walimwengu. Swalah na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah wote.

Baraza la Kibaar-ul-´Ulamaa´ katika mji wa Riyaadh tarehe 16-07-1441 wamedurusu hukumu ya kuacha kuhudhuria swalah ya ijumaa na swalah ya mkusanyiko kutokana na janga au khofu ya kuenea kwake. Baada ya kudurusu maandiko ya Shari´ah ya Kiislamu na malengo yake na misingi yake na maneno ya wanachuoni juu ya masuala haya, basi kamati ya Kibaar-ul-´Ulamaa´ wanabainisha yafuatayo:

1- Ni haramu kwa mwambukizwa kuhudhuria swalah ya ijumaa na swalah ya mkusanyiko. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mgonjwa asimwendee mwenye afya njema.”[1]

“Mkisikia kuhusu tauni katika mji fulani, basi msiingie ndani yake. Na kikitokea katika mji fulani na nyinyi mko ndani yake, basi msitoke ndani yake.”[2]

2- Yule ambaye mamlaka itamweka karantini basi ni lazima kwake kukubali jambo hilo na asihudhurie swalah ya mkusanyiko na swalah ya ijumaa. Katika hali hiyo ataswali nyumbani kwake au mahala alipowekwa karantini. ash-Shurayd bin Shariyk ath-Thaqafiy amesema:

“Katika kikosi cha Thaqafiy alikuwa bwana mmoja mwenye ugonjwa wa ukoma. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamtumia ujumbe: “Tumepokea kiapo chako. Rejea.”[3]

3- Yule anayeogopa asije kuambukizwa au kuwaambukiza wengine basi ana ruhusa ya kutohudhuria swalah ya ijumaa na swalah ya mkusanyiko. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna madhara wala kudhuriana.”[4]

Yule asiyehudhuria swalah ya ijumaa basi badala yake atatakiwa kuiswali Dhuhr Rak´ah nne.

Kibaar-ul-´Ulamaa´ inawahimiza watu wote kushikamana na maamrisho na maelekezo yanayotoka kwenye mamlaka pamoja na kumcha Allaah (´Azza wa Jall) na kurejea Kwake kwa kumuomba du´aa na kunyenyekea mbele Yake ili aondoshe janga hili. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَإِن يَمْسَسْكَ اللَّـهُ بِضُرٍّ فَلَا كَاشِفَ لَهُ إِلَّا هُوَ ۖ وَإِن يَمْسَسْكَ بِخَيْرٍ فَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

“Allaah akikugusisha kwa dhara, basi hakuna yeyote wa kukuondolea nalo isipokuwa Yeye; na akikugusisha jambo jema, basi Yeye juu ya kila jambo ni muweza.”[5]

وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ

”Mola wenu amesema: “Niombeni Nitakuitikieni.”[6]

Swalah na salamu zimwendee Mtume wetu Muhamamd, kizazi chake na Maswahabah zake.

[1] al-Bukhaariy na Muslim.

[2] al-Bukhaariy (5729) na Muslim (2218).

[3] Muslim.

[4] Ibn Maajah (2341), Ahmad (5/327) na al-Haakim (2345) aliyeisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[5] 06:17

[6] 40:60

  • Mhusika: Kibaar-ul-´Ulamaa´
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://twitter.com/makkahregion/status/1238110624745390080
  • Imechapishwa: 12/03/2020