Swalah ya anayetokwa na upepo mara kwa mara


Swali: Nasumbuliwa na maradhi sugu kwenye koloni ambayo husababisha kutokwa na harufu mbaya na khaswa ndani ya swalah. Kutokana na wingi wa kutoka kwake nimekuwa mwenye kutilia shaka swalah yangu hata nikihisi harufu kutoka upande mwingine wowote basi hudhani kuwa ni yenye kutoka kwangu. Nifanye nini ndani ya swalah? Je, ni lazima kwangu kutawadha wakati ninapopatwa na mashaka? Je, inafaa kwangu kuwa imamu katika hali ambayo maamuma hawajui kisomo?

Jibu: Msingi ni kubaki kwa twahara. Ni lazima kwako kukamilisha swalah na kutojali wasiwasi mpaka utambue kwa yakini kwamba umetokwa na kitu kwa kusikia sauti au kupatikana kwa harufu ambayo kuna uhakika ni yenye kutoka kwako. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema wakati alipoulizwa juu ya mtu anayehisi kitu ndani ya swalah akasema:

“Asiondoke mpaka asikie sauti au ahisi harufu.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Hapana neno ukawa imamu ukiwa ndiye msomaji zaidi ya wale wahudhuriaji wengine. Hapa ni pale ambapo hadathi itakuwa si endelevu bali inakujia baadhi ya nyakati. Pale unapopatwa na hadathi basi swalah inabatilika. Ni mamoja uko imamu, maamuma au unaswali peke yako. Pindi utapopatwa na hadathi ilihali ni imamu basi achukue nafasi yako mmoja katika wale unaowaswalisha miongoni mwa waswaliji maalum walioko nyuma yako.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/121)
  • Imechapishwa: 19/08/2021