Swalah nyingi za faradhi kwa wudhuu´ mmoja

Swali: Je, inajuzu kwa mtu kuswali faradhi nyingi kwa wudhuu´ mmoja ikiwa hakupatwa na hadathi? Je, anayefanya hivo anapata fadhilah za Hadiyth:

“Mnaonaje lau kama kuna mto wa maji unaopita mbele ya nyumba ya mmoja wenu, ambamo, mwenye nyumba hiyo, anaoga mara tano kwa siku. Je, anaweza mtu huyo kubakiwa na taka mwilini mwake?” Wakasema: “Hapana! Haiwezekani kuabakiwa na taka mwilini mwake.” Ndipo akasema: “Basi na swalah tano nazo ni vivyo hivyo! Allaah anafuta, kwa swala hizo, dhambi zote za mwenye kuziswali.”?

Jibu: Inajuzu kwa mtu kuswali swalah mbili, tatu, nne, tano au sita kwa wudhuu´ mmoja. Imethibiti ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku ya Ufunguzi aliswali swalah tano kwa wudhuu´ mmoja. ´Umar akamwambia: “Umefanya kitu ambacho hukuwa ukikifanya, ee Mtume wa Allaah?” Akasema:

“Nimefanya kwa makusudi, ee ´Umar.”

Bi maana ili nibainishe kufaa kwake. Kwa hiyo ni sawa kwa mtu akibaki na wudhuu´ basi auswalie swalah nyingi. Lakini akitia wudhuu´ upya ndio bora zaidi na khaswa kama amepatwa na uvivu au usingizi. Vinginevyo hakuna neno.

Imepokelewa katika baadhi ya Hadiyth, ingawa kuna unyonge ndani yake, ya kwamba:

“Yule ambaye atatawadha ingawa yuko na twahara, basi atakuwa na mema kumi.”

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Mutanawwi´ah (18)
  • Imechapishwa: 30/01/2021