Swali: Je, kuna swalah kwa ajili ya wazazi wawili waliokwishakufa na inaswaliwa namna gani?

Jibu: Watoto hakuna juu yao swalah kwa wazazi wawili baada ya kufa wala wasiokuwa wazazi. Kilichowekwa katika Shari´ah ni kuwaombea du´aa, kuwaombea msamaha, kuwatolea swadaqah, kuwahijia na kuwafanyia ´umrah. Kuhusu swalah haikusuniwa kwa yeyote kuswali kwa ajili ya yeyote. Anayeswaliwa ni maiti wa kiislamu kabla ya kuzikwa kwake. Yule ambaye hakuwahi kumswalia kabla ya kuzikwa basi imesuniwa kwake kumswalia baada ya kuzikwa akiwa kile kipindi hakizidi takriban miezi mitatu. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliswalia kaburi la mama yake na Sa´d bin ´Ubaadah baada ya kupita mwezi mmoja. Vivyo hivyo Sunnah ya Twawaaf ambayo ni zile Rak´ah mbili baada ya Twawaaf zimesuniwa kwa mwenye kutufu. Miongoni mwa hayo ni kumfanyia mwingine hajj au ´umrah. Ni jambo limewekwa katika Shari´ah akimfanyia Twawaaf kwa niaba ya mwakilishi wake akamswalia Rak´ah mbili zinazofuatia ile Twawaaf. Msingi wa yote hayo ni kwamba ´ibaadah ni jambo la kukomeka; hakukubaliwi katika Shari´ah isipokuwa yale yaliyothibiti ndani ya Qur-aan na Sunnah.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (11/418)
  • Imechapishwa: 18/08/2022