Siwaak inatumiwa kwa mkono wa kulia au wa kushoto?

Swali: Mtu anatakiwa kutumia Siwaak kwa mkono wa kulia au kwa mkono wa kushoto?

Jibu: Wanachuoni wametofautiana. Wapo wanachuoni wenye kuona kuwa mtu aswaki na mkono wa kulia. Hoja yao ni kwamba Siwaak  ni katika Sunnah na kumtii Allaah. Kwa hivyo haistahiki kutumia mkono wa kushoto. Kwani mkono wa kushoto ni wenye kutumiwa katika kuondosha vitu vibaya.

Wanachuoni wengine wakasema kuwa bora ni kutumia mkono wa kushoto. Hoja yao ni kwamba mkono wa kushoto ni wenye kutumiwa kuondosha vitu vibaya. Vitu vibaya vinatakiwa kuondoshwa kwa mkono wa kushoto. Wakasema ni kama mfano wa kujisafisha chooni kwa maji na kwa mawe. Kunatumiwa mkono wa kushoto na sio mkono wa kulia.

Wanachuoni wengine wakapambanua na kusema kuwa endapo mtu ataswaki kwa ajili ya kusafisha mdomo, kama mtu ndio ameamka kutoka usingizini au anaswaki kwa ajili ya kuondosha uchafu, katika hali hii anatakiwa kutumia mkono wa kushoto kwa sababu inahusiana na kuondosha uchafu. Na endapo mtu ataswaki kwa ajili ya kutaka kupata Sunnah basi katika hali hiyo atumie mkono wa kulia. Kwa sababu ni kutaka kujikurubisha tu. Ni kama mfano mtu alitawadha na kuswaki karibuni tu, basi aswaki kwa mkono wa kulia. Jambo hili ni pana. Mtu atumie Siwaak vile anavyotaka kwa sababu katika masuala haya hakuna andiko la wazi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (11/115-116)
  • Imechapishwa: 16/06/2017