Sigara inachengua wudhuu´?


Swali: Mtu akiwa ameshatawadha kisha akavuta sigara na kuswali moja kwa moja na huenda mtu huyu akawaongoza watu katika swalah. Tumemwambia aliyefanya hivo kwamba sigara inachengua wudhuu´ ambapo akatujibu kuwa si kweli. Ni ipi hukumu ya hilo?

Jibu: Sigara haichengui wudhuu´. Lakini hata hivyo ni haramu na chafu. Ni wajibu kuiacha. Lakini mtu akivuta na akaswali swalah yake haiharibiki na wala wudhuu´ wake hauchenguki. Ni aina fulani ya majani yanayotambulika. Lakini ni haramu kutokana na madhara yake. Ni wajibu kwa yule mwenye kuivuta atahadhari nayo, aiache na aiogope shari yake. Haijuzu kwake kuiuza wala kuitumia. Bali ni wajibu kwa yule mwenye kuitumia kutubu kwa Allaah na aache kufanya nayo biashara. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَسْأَلُونَكَ مَاذَا أُحِلَّ لَهُمْ ۖ قُلْ أُحِلَّ لَكُمُ الطَّيِّبَاتُ

“Wanakuuliza wamehalalishiwa nini? Sema: “Mmehalalishiwa vilivyo vizuri.”[1]

Hatukuhalalishiwa isipokuwa vizuri na vyakula vizuri. Allaah (Subhaanah) hali ya kumsifu Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

وَيُحِلُّ لَهُمُ الطَّيِّبَاتِ وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَائِثَ

“Anawahalalishia vilivyo vizuri na anawaharamishia vichafu.”[2]

Hapana shaka yoyote kwamba sigara na vya kulevya vyote ni katika machafu. Hali kadhalika bangi pia ni katika machafu. Ni wajibu kuachana nayo.

Vivyo hivyo mirungi inayotambulika huko Yemen ni katika machafu. Kwa sababu ina madhara makubwa. Kwa sababu inadhuru madhara makubwa, kuharibu wakati na kupoteza swalah. Ni wajibu kwa yule mwenye kuitumia kuachana nayo, kutubia kutokamana na hayo, aichunge afya yake, mali yake na wakati wake katika mambo yenye kumnufaisha. Kwa sababu lililo wajibu kwa muumini ni yeye kutahadhari yenye kumdhuru katika dini na dunia yake. Ni wajibu kwa mtu kutahadhari mfano wa sigara na vitu vyengine vyote vyenye kulevya. Pamoja vilevile atubie tawbah ya kweli juu ya yale yote yaliyotangulia. Haijuzu kufanya biashara ya vitu hivyo. Bali ni wajibu kuachana na hayo na kutofanya biashara na vitu hivyo. Kwa sababu vinawadhuru waislamu.

[1] 05:04

[2] 07:157

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Fataawaa (10/162) https://binbaz.org.sa/fatwas/3798/%D9%87%D9%84-%D8%A7%D9%84%D8%AF%D8%AE%D8%A7%D9%86-%D9%8A%D9%86%D9%82%D8%B6-%D8%A7%D9%84%D9%88%D8%B6%D9%88%D8%A1