Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

12- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Moja ya sifa nzuri za muislamu ni kuachana na yale yasiyomuhusu.”

Hadiyth hii ni miongoni mwa Hadiyth kubwa za adabu. Inatupaswa kwetu, kwa njia ya uwajibu, kuwa na pupa katika kuufanya Uislamu [wetu] kuwa mzuri. Kwa sababu katika kufanya hivo ndani yake kuna fadhila kubwa. Miongoni mwa sifa nzuri za Uislamu ni sisi kuachana na yale yasiyotuhusu, sawa ikiwa ni katika maneno, kusikia, tusiulize maswali yasiyokuwa na maana, tusipekue khabari za watu ambazo hatuna faida nazo: huyu amefanya, huyu ameacha, huyu ameenda, huyu amekuja na kadhalika. Yote haya ni yenye kulaumika na yanamfanya mtu kutoufanya Uislamu wake kuwa mzuri endapo yatakithiri kwake.

Kutokana na hili tunasema, katika Hadiyth hii kuna wasia mkubwa katika adabu hii kubwa ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakika moja katika sifa nzuri za muislamu ni yeye kuachana na yale yasiyomuhusu katika Dini yake, mambo yake ya dunia, maneno, matendo na mfano wa hayo.

  • Mhusika: Shaykh Swaalih bin ´Abdil-´Aziyz Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Arba´iyn an-Nawawiyyah, uk. 216
  • Imechapishwa: 15/05/2020